KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Friday, April 10, 2015

BENKI YA TWIGA BANCORP YATANGAZA MIPANGO NA MALENGO YA KUIPAISHA KIUFANISI NCHINI.

 Mgeni rasmi Msajili wa Hazina,Laurence Mafuru (wa pili kushoto waliokaa)
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Twiga Bancorp,Profesa Ammon Mbelle (katikati) na Afisa Mtendaji Mkuu,Cosmas Kimario  na Dome Malosha (kushoto waliokaa) wa Ofisi ya Msajili Hazina wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya benki hiyo.
 Wajumbe wa Bodi ya Benki hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Mgeni rasmi Msajili wa Hazina,Laurence Mafuru (kushoto),akizungumza na waandishi,Wajumbe Bodi ya Wakurugenzi Twiga Bancorp Ltd na Menejimenti kuhusu mipango na malengo ya Benki hiyo mwishoni mwa wiki.Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Twiga,Profesa Ammon Mbelle (katikati) na Afisa Mtendaji Mkuu,Cosmas Kimario.
 Wajumbe wa Bodi wakifuatilia katika mkutano na waandishi.
 Mgeni rasmi Msajili wa Hazina,Laurence Mafuru (wa pili kushoto),akizungumza na waandishi,Wajumbe Bodi ya Wakurugenzi Twiga Bancorp Ltd na Menejimenti kuhusu mipango na malengo ya Benki hiyo mwishoni mwa wiki.Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Twiga,Profesa Ammon Mbelle (katikati) na Afisa Mtendaji Mkuu,Cosmas Kimario.Dome Malosha (kushoto) wa Ofisi ya Msajili Hazina.
 Mgeni rasmi Msajili wa Hazina,Laurence Mafuru akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Twiga,Profesa Ammon Mbelle
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Twiga,Profesa Ammon Mbelle (kulia) akimkabidhi zawadi Dome Malosha (kushoto) wa Ofisi ya Msajili Hazina.
 Mgeni rasmi Msajili wa Hazina,Laurence Mafuru(kushoto) akizungumza na baadhi ya wajumbe wa Bodi. 


MAELEZO YA MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI YA TWIGA BANCORP LIMITED, PROF. AMMON V.Y. MBELLE, KWA MSAJILI WA HAZINA TAREHE 10 APRILI 2015, MAKAO MAKUU YA TWIGA BANCORP DAR ES SALAAM.

Ndugu Laurence Mafuru, Msajili wa Hazina,
Ndugu Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Twiga Bancorp Ltd,
Ndugu Cosmas T. Kimario, Mkurugenzi Mtendaji (CEO) Twiga Bancorp Ltd,
Ndugu Mwenyekiti wa Tawi la TUICO, Twiga Bancorp Ltd
Menejimenti ya Twiga Bancorp,
Wafanyakazi wa Twiga Bancorp,
Waandashi wa Habari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Habari za asubuhi
Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi wa Twiga Bancorp Limited na kwa niaba yangu binafsi napenda kwa heshima kubwa kukushukuru wewe Msajili wa Hazina kwa ujio wako wenye nia ya kusikiliza hali ya Twiga Bancorp, chombo cha wananchi wa Tanzania na pia kutupatia maelekezo juu ya matarajio yako kwa Twiga Bancorp Ltd. Tumefarijika sana kwani fursa hii haijawahi kutokea tangu TBCL ilipoanzishwa tarehe 1 Novemba mwaka 2004. Tunakuahidi kuwa tutasikiliza kwa umakini mkubwa na kutekeleza kwa weledi kamilifu maelekezo yako ili matarajio ya Mwenye Hisa na Watanzania kwa ujumla juu ya TBCL yaweze kukidhiwa.
Pili, Bodi ya Twiga Bancorp Ltd, kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote kwa ujumla tunapenda kutoa shukurani zetu za dhati kupitia kwaqko, kwa Serikali ambayo ni mwenye hisa pekee,  kwa kushikamana na benki hii, ikiwa ni pamoja na kuiongezea mtaji pale hali ya kifedha inaporuhusu.
Pia nitoe shukrani za pekee kwa wadau wetu mbalimbali waliotuwezesha kufika hapa tulipo katika mazingira ya ushindani mkubwa wa kibenki ambao upo sasa nchini mwetu. Kuna msemo wa Kichina usemao “ukitaka kwenda safari fupi, nenda pekee yako lakini ukitaka kwenda safari ndefu nenda na wenzako”. Benki ya Twiga inataka kwenda safari ndefu na ndio maana inathamini sana wadau wake, wakiwemo wateja wa benki ambao ni wananchi wa kipato cha chini.
Ndugu Msajili wa Hazina,
Katika mfumo bora wa utawala, nafasi na majukumu ya Bodi ya Wakurugenzi wasio watendaji, katika ulimwengu wa sasa ni kuweza kuainisha mahitaji ya sasa.  Bodi ya Wakurugenzi ni mhimili mkubwa katika utawala bora; ikiwajibika kwa wenye hisa kwa kusimamia utendaji wa taasisi husika katika utawala bora, uwazi, uwajibikaji, nidhamu, na uadilifu, lakini ikiepuka kishawishi cha kujihusisha moja kwa moja na shughuli za kiutendaji wa Shirika. Utawala bora wa kibenki umeoneshwa pia kwa Mwenyekiti wa Bodi kutokuwa mjumbe wa Kamati za Bodi kadiri ya maudhui ya “King III”.
Katika kutekeleza majukumu yake Bodi ya Twiga Bancorp imepitisha Sera mbalimbali na na kupitisha mikakati inayolenga kukuza mtaji wa benki, na kuongeza ubora wa huduma kwa wateja wa benki na kuleta mshikamano kwa wafanyakazi wa benki. Bodi imekuwa ikiwasimamia wafanyakazi ili waongeze ari mpya katika utendaji wao wa kazi wakizingatia maudhui ya umoja na kubadilika kifikra katika utendaji kazi kwani kufanya kazi kwa mazoea hakuna nafasi katika zama za sasa za ushindani wa kibenki. Aidha Bodi imeendelea kuwasisitiza watendaji wakuu na wafanyakazi wote kuwa wamepewa dhamana na Watanzania karibu milioni 45, kuilea na kuikuza benki hii; hivyo uadilifu na weledi ni muhimu katika wajibu huo. Bodi ya Wakurugenzi haijasita hata mara moja kuwachukulia hatua za kinidhamu wafanyakazi wanapokiuka hayo, bila kujali ngazi zao za utumishi.
Ndugu Msajili wa Hazina,
Twiga Bancorp ni benki pekee nchini inayotekeleza dhama ya ujumuiashi “financial inclusion” katika kutoa huduma za kibenki. Wateja wake wakubwa ni wale wa vipato vya chini. Tumetambulika kimataifa kwa utoaji bora wa huduma hiyo na kupata tuzo mbalimbali za Kimataifa: kwa mfano mwaka 2012 na mwaka 2015 Twiga Bancorp ilikuwa mshindi wa kwanza na ilitunukiwa Tuzo ya kiwango cha dhahabu kimataifa inayotolewa Geneva Uswisi kwa kuwa benki bora katika utoaji huduma ndani na nje ya nchi. Haya si mafanikio madogo.
Baadhi ya mafanikio yaliyotokana na usimamizi thabiti wa Bodi ya Wakurugenzi ni pamoja na:
1.    Kuongeza mtandao wa kutoa huduma nchini toka kituo kimoja mwaka 2004 hadi kufikia kumi yakiwemo matawi kamili matano; ikiwa ni pamoja na kwenda sehemu za pembezoni; kuongeza idadi ya wateja kutoka 20,551 mwaka 2005 hadi wateja 35,953 mwaka 2015 likiwa ni ongezeko la asilimia 71%.

2.    Kuanzisha Baraza la Wafanyakazi kwa kulizingatia Sheria za nchi zinazotamka  kuwepo kwa Baraza la Wafanyakazi  linaongozwa kwa mujibu wa Sheria, lakini kwa mapana zaidi kutambua umuhimu wa kuwepo kwa Baraza (kwani kabla ya hapo halikuwepo) na wajibu wa Baraza hilo. Pia Baraza hilo limeelekezwa kusimamia haki na wajibu na kudhibiti vitendo visivyo na maadili

3.    Kujiunga na mtandao wa UMOJA SWITCH ambao kwa sasa una mabenki 28 yaliyosambaa nchi nzima. Mtu yeyote mwenye akaunti na Twiga Bancorp anaweza kuchukua fedha toka akaunti yake kwenye benki yoyote katika hizo benki 28. Twigabancorp ni benki ya pili kwa kutoa huduma hii ya UMOJA SWITCH;


4.    Kujenga miundombinu ya kuwezesha matumizi ya teknolojia ya hali ya juu katika kutoa huduma kupitia mtandao mpya ujulikanao kama SAB. Hii itaongeza ufanisi katika kuto huduma kwa haraka, usalama na kwa wakati; na kuweza kuwafikia wateja wetu popote; ndani na nje ya nchi;

5.    Kuunganisha jitihada za benki na Mwenye Hisa, Msimamizi wa Mabenki nchini, Benki Kuu ya Tanzania; vyombo vya kutunga na Kusimamia Sheria;

6.    Kutia uhai mpya “invigorate” katika Menejimenti.

Aidha Bodi ya Wakurugenzi imezingatia sana gharama za uendeshaji wake. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano hatujaongeza posho za aina yeyote kwa Wakurugenzi wa Bodi; wala kuunga msululu kwenye safari za Menejimenti nje na ndani ya nchi. Pili iliahirisha sherehe ya miaka kumi ya Banki ili kubana matumizi.
Ndugu Msajili wa Hazina
Tunapenda pia kukuarifu kwamba Twiga Bancorp Limited inashiriki katika huduma za kijamii. Twiga Bancorp imeshiriki katika huduma mbalimbali kama vile kutoa misaada kwa wathirika wa majanga mbalimbali kama waathirika wa mabomu Mbagala, vituo vya kulelea yatima na kadhalika. Vile vile Twigabancorp Limited imekuwa ikichangia kwenye uzunduzi wa vikundi vya VIKOBA. Ni matarajio ya Bodi kuwa wajibu huo utaendelea kadiri hali ya kifedha itakavyoruhusu.

Ndugu Msajili wa Hazina
HUDUMA BORA NDIYO FAHARI YETU TWIGA BANCORP. Katika kutekeleza majukumu hayo benki inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo:
  1. Mtaji mdogo
  2. Kutokuwa na jengo letu la kiofisi kwa Makao Makuu na tawi la Dodoma; hivyo kulazimika kupanga kwa gharama kubwa.
  3. Kurundikana kwa kesi zetu za madai katika vyombo vya Sheria na Haki. Kwa hili tunapendekeza kuanzishwa “Mahakama ya Mabenki” ikizingatiwa changamoto za kisasa zinazokabili mabenki mfano wizi wa mtandao “cyber crimes” na pia kutotosheleza kwa Mahakama ya Kibiashara katika jambo hili.

Prof. A.V.Y. Mbelle (Ph.D)
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
Twiga Bancorp Limited
10 Aprili, 2015


TAARIFA YA AFISA MTENDAJI MKUU WA TWIGA BANCORP LIMITED BW. COSMAS T. KIMARIO KWA MSAJILI WA HAZINA TAREHE 10 APRILI 2015, MAKAO MAKUU YA TWIGA BANCORP DAR ES SALAAM.

Ahsante ndugu Mwenyekiti,
Ndugu Msajili wa Hazina, Ndugu Mwenyekiti wa Bodi, Ndugu Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Twiga Bancorp Ltd, Ndugu Mwenyekiti wa tawi la TUICO, Twiga Bancorp Ltd, Menejimenti ya Twiga Bancorp, Waandashi wa Habari, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.
1.0 Mipango na Malengo ya Benki
Ifuatayo ni mipango na malengo ya benki kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2018:
  • Kuibadilisha benki kutoka taasisi inayopata hasara na kuwa taasisi inayopata faida.
  • Kukuza mikopo kwa 25%; Kutoka Tsh 40 billioni mwaka 2014 hadi kufikia Tsh 96 billioni ifikapo mwaka 2018.
  • Kupunguza mikopo chechefu kutoka 21% kwa sasa hadi kufikia 5% mwaka 2018.
  • Kukuza amana za wateja hadi kufikia 35% kwa mwaka; Kutoka Tsh 56 billioni mwaka 2014 hadi kufikia Tsh 187 billioni mwaka 2018.
  • Kuboresha vitabu vyetu vya hesabu kwa 21%; Kutoka Tsh 80 billioni mwaka 2014 hadi kufikia Tsh 175 billioni mwaka 2018.
2.0 Mpango Mikakati
Ndugu Msajili wa Hazina, Waandishi wa Habari, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana
Katika kufikia mipango na malengo tajwa hapo juu, benki imejiwekea mpango mikakati ifuatayo:
  • Kutekeleza kwa ufanisi mpango mkakati biashara wa benki wa mwaka 2015.
  • Kupitia mpango mkakati biashara wa benki mara kwa mara na kufanya utekelezaji kulingana na mazingira na mahitaji yatakayojitokeza.
  • Kuongeza mapato ya benki kwa kuanzisha bidhaa na huduma mpya.
  • Kutafuta vyanzo vingine vikuu vya mapato ambavyo havitaiyumbisha benki kibiashara.
  • Kujenga mahusiano mazuri kibishara na Taasisi, Makampuni na Masharika ya ndani ya  nchi na yale ya nje ya nchi.
  • Kusimamia kwa umakini na kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa wakati kama ilivyoainishwa kwenye mpango mkakati biashara wa benki.
  • Kuanzisha na kutekeleza utaratibu maalum wa kupima utendaji wa kazi kwa Wafanyakazi na Menejimenti ya benki katika idara zote.
  • Kufuatilia mikopo sugu. Hii ikiwa ni pamoja na kupiga mnada mali za wateja sugu.
  • Kukuza mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ikiwemo VICOBA vilivyo chini ya asasi ya UYACODE NA DMI.
  • Kuendeleza mazungumzo na wajasiriamali wadogo na wakati ili wafungue akaunti zao za biashara Twiga Bancorp.
Mpango mikakati huu umeanza kuleta tija kwani katika robo ya kwanza ya mwaka huu benki imeweza kupata faida kabla ya kodi Tsh 174 millioni ukilinganisha na lengo lililowekwa la                                                                                                                                                                                                                            kupata faida ya Tsh 104 millioni.
Hatua nyingine zinazochukuliwa na benki katika kufikia malengo tajwa hapo juu ni pamoja na:
v  Kubadilisha Muundo wa kampuni yaani ‘Organizational Sturucture’ ili kuleta tija na ufanisi zaidi katika utendaji. Zoezi hili limefanyika katika robo ya kwanza ya mwaka huu 2015.
v  Katika robo ya pili ya mwaka 2015, benki inategemea kupata mtaji zaidi kutoka kwa Mmiliki Mkuu. Kukua kwa mtaji kutawezesha benki kubadili hadhi yake na kuwa benki kamili ya kibiashara yaani ‘Fully Fledged Commercial Bank’. Hatua hii itawezesha benki kufungua matawi mengi zaidi nchi nzima.
v  Kumalizia ufungajii wa mfumo wa komputa imara zaidi na madhubuti katika kutoa huduma mbalimbali za kibenki. Hii pia itawezesha benki kutoa huduma bora zaidi na mpya kwa wateja kama: Mobile Banking, Internet banking, Agency Banking n.k.
v  Kusogeza huduma zetu karibu zaidi na wanachi kwa kupitia vituo vya uwakala.



3.0 Hitimisho
Wito na Ombi
Ndugu Msajili wa Hazina, Waandishi wa Habari, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana
Kwa mafanikio haya ambayo benki imepata na mpango mikakati kabambe tuliyonayo napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa Taasisi, Makampuni, Mashirika ya Serikali na Watu Binafsi na Wananchi wote kwa ujumla kuitumia Twiga Bancorp katika shughuli mbalimbali za kibenki kwani riba zetu ni nzuri na za kuvutia, huduma zetu ni bora na pia benki hii inamilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja (100%). Hii itawezesha benki yetu kukua na kupata mafanikio makubwa zaidi na hivyo kuisaidia serikali katika jitihada zake za kupambana na umaskini. Tujivunie kilicho chetu!!


Ahasanteni sana kwa kunisikiliza

Cosmas T. Kimario
Afisa Mtendaji Mkuu
Twiga Bancorp Limited
10 Aprili, 2015


No comments: