Katika
hali ya kushangaza na kusikitisha tarehe 6/09/2015 siku ya Jumapili
mjini Tabora mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Chadema Ndg. Edward Lowassa aliamua kutumia udini kuomba kura.
Ndg.
Lowassa akihudhuria ibada katika kanisa la Kilutheri (KKKT) mjini
Tabora amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya
kijamii akidai kuwa, kwa kuwa toka nchi ipate uhuru hajawahi kutokea
Rais kutoka dhehebu la Kilutheri hivyo mwaka huu ni zamu ya Walutheri.
Chama
Cha Mapinduzi kinalaani matumizi ya lugha zinazoligawa Taifa letu kwa
misingi ya udini, ukanda, ukabila na ubaguzi wa aina yeyote kisa tu
kutafuta madaraka.
Kauli hii ya Ndg. Lowassa licha ya kuwa ni
kinyume na Sheria za Uchaguzi za nchi yetu, kinyume na Kanuni za Maadili
ya Uchaguzi zilizosainiwa na vyama vyote, lakini ni kinyume kabisa na
mila na desturi za Kitanzania katika kuhakikisha Taifa hili linabaki
kuwa Taifa moja lenye umoja, amani na mshikamano.
Kwa mfano,
Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015,
yaliyotolewa na Tangazo la Serikali Na. 294 la tarehe 27/7/2015 chini ya
kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, ukurasa
wa 5 kifungu 2.1(k) kinasema:-
"Viongozi wa vyama
vya siasa, wagombea au wafuasi wao wahakikishe kuwa majengo wanayotumia
kufanya kampeni sio ya Ibada. Vile vile, vyama vya siasa vihakikishe
kuwa havitumii viongozi wa dini kupiga kampeni kwa ajili ya vyama vya
siasa au wagombea wao".
Lakini katika maadili hayo hayo, ukurasa wa 7, kifungu 2.2(i) kinasema:-
"Vyama vya siasa au Wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa kura
kwa misingi ya UDINI, UKABILA, JINSIA AU RANGI."
Kwa
kuwa Ndg. Lowassa siku hizi tabia ya kusahau inaongezeka kwa kasi
nimeona ninukuu vifungu hivi kwa rejea yake na wenye tabia kama yake.
Lakini
matamshi hayo ni uthibitisho tosha kuwa Ndg. Lowassa, Chama chake cha
CHADEMA na vyama vinavyomuunga mkono chini ya UKAWA ni wabaguzi,
wachochezi na waroho wa madaraka wasiojali masilahi mapana ya nchi yetu.
Kwao madaraka ni muhimu kuliko nchi yetu.
Hii si mara ya kwanza
kwa Ndg. Lowassa, Chama chake cha CHADEMA na makada wenzake kutoa kauli
na kufanya vitendo vya kibaguzi, kwa kutumia ukanda na sasa wameamua
kutumia udini kama njia ya mkato ya kutafuta madaraka.
Chama Cha
Mapinduzi kinaamini huu si msimamo wala utamaduni wa Watanzania, bali ni
uroho binafsi wa madaraka wa Ndg. Lowassa na chama chake, hasa baada ya
kuona kuwa hoja zake za kutafuta nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa
nchi yetu zimekataliwa na wananchi.
Mwalimu aliwahi kutuonya juu
ya wanasiasa wanaotumia udini na ukabila kama hoja ya kutaka kupata
madaraka kuwa ni wanasiasa walifilisika kisiasa lakini ni watu wa hatari
sana kwa mustakabali wa amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu.
Hivyo
basi, Chama Cha Mapinduzi kinalaani kauli hii na tunaamini inapaswa
kulaaniwa na wote wanaoipenda nchi yetu. Lakini CCM inaamini vyombo
vinavyohusika na hasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itachukua hatua
zinazostahili kuondoa mbegu hii ya kansa inayoletwa na Ndg. Lowassa
kwenye nchi yetu. Maneno ya Ndg. Lowassa ni kansa mbaya kwa nchi yetu na
lazima yakemewe na kukomeshwa kabisa.
Maneno na
vitendo vya Ndg. Lowassa, chama chake, na makada wenzake wa CHADEMA na
vyama shirika vya UKAWA toka wameanza kampeni katika maeneo mbalimbali
ya nchi yetu na kwa nyakati tofauti zimejaa ghiriba na ubaguzi
uliokithiri. Tabia hizi za Ndg. Lowassa ni moja ya sababu iliyopelekea
CCM kutompa nafasi ya kugombea kupitia Chama hichi.
CCM inatoa
wito kwa wadau wote na Watanzania wote kuwa ni vizuri kuwa makini wakati
huu wa Uchaguzi, kuhakikisha hakuna jambo linaligawa Taifa letu.
Tuendeshe kampeni bila kuligawa na kuliangamiza Taifa letu. Tanzania yetu ni muhimu. Tanzania kwanza mengine baadae.
Imetolewa na;-
No comments:
Post a Comment