Mratibu wa Mradi wa kuzalisha gesi ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa 4
katika fani ya Uhandisi wa Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi John
Rutahirwa Akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu moja ya mtambo
wa kukusanyia maji taka kutoka majumbani eneo la mradi wa
kuzalisha gesi Vingunguti.Gesi hiyo itaanza kutumika mwezi Desemba mwaka
huu.
Meneja Uhusiano wa DAWASCO Bi.Neli Msuya (kulia) akiwa na Mtaalam
anayehusika na ujenzi, mafunzo na usimamizi wa mfumo wa mradi wa
kuzalisha Gesi Vingunguti ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa nne wa
shahada ya Uhandisi wa Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi Rukia Yange
wakionyesha moja ya kifungashio cha Gesi itakayotumika majumbani
Kutokana na maji taka yanayokusanywa eneo la Vingunguti.Mradi
huo unalenga kuwapunguzia wananchi gharama za uhifadhi wa maji taka
na kuwapatia nishati ya gesi kwa gharama nafuu itakayowasaidia
kuondokana na matumizi ya mkaa.
Jumanne Saidi Fundi ujenzi wa vyoo na msimamizi wa mradi wa majaribio
wa Biogasi Vingunguti akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu
kazi ya ufungaji wa miundombinu ya kuzalisha gesi katika eneo la
Vingunguti.
Moja ya choo cha kisasa kilichojengwa katika moja ya familia kwa ajili ya mradi wa kuzalisha Gesi katika eneo la Vingunguti.
Eneo la Mtaa wa mji mpya Vingunguti ambako mabomba ya kupitishia
maji taka kutoka kwenye vyoo vya wananchi ambayo huenda moja kwa moja
kwenye mtambo wa kuzalishia Gesi.
Mtambo wa kuzalisha Gesi katika katika eneo la Mradi wa Majaribio eneo
la Vingunguti unaokusanya maji taka moja kwa moja kutoka katika makazi
ya wananchi.Mtambo huo kwa mujibu wa maelezo ya watalaam wa mradi huo
una uwezo wa kukaa ardhini kwa kipindi cha miaka 50.(Picha na Aron Msigwa - MAELEZO).
Na.Aron Msigwa - MAELEZO.
Dar es salaam.
Wakazi
wa mtaa wa mji mpya, kata ya Vingunguti, Manispaa ya Ilala jijini Dar
es salaam wako mbioni kuanza kunufaika na mradi wa uzalishaji wa Gesi
inayotokana na maji taka ya vyoo vyao na yale ya yaliyo katika mabwawa
makubwa ya kuhifadhia maji taka yaliyo katika eneo hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika eneo unapojengwa mradi wa majaribio wa
kuzalisha Gesi, Mratibu wa Mradi huo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka
wa 4 katika fani ya Uhandisi wa Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi John
Rutahirwa amesema kuwa wananchi wataanza kutumia gesi itakayozalishwa
kuanzia mwezi Desemba mwaka huu.
Amesema kazi
ya kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya mradi huo inaendelea chini ya
usimamizi wa Mamlaka ya Maji Taka (DAWASA) kwa kushirikiana na Wanafunzi
wa fani ya Uhandisi wa Chuo Chuo Kikuu cha Ardhi na Taasisi isiyo ya
kiserikali ya wanafunzi wanaosomea fani ya uhandisi wa Mazingira (CDI)
ya Chuo kikuu cha Cambridge, Uingereza.
Amesema
wanafunzi wanaosomea fani ya Uhandisi wa Mazingira wa Chuo Kikuu cha
Cambridge,Uingereza kwa kushirikiana na baadhi ya wanafunzi wanaosomea
Uhandisi wa Mazingira wa Chuo Kikuu cha Ardhi nchini Tanzania walikuja
na wazo na kubuni mradi huo wenye lengo la kuboresha maisha kupitia maji
taka.
Amesema chini ya uratibu wa DAWASA yenye
jukumu la kusimamia miundombinu ya maji taka na Taasisi ya mikopo la
Bridge for change ya Tanzania inayotoa mikopo midogo midogo kwa
wananchi walianza kufanya mapitio kwa kila nyumba ili kuona namna
wanavyoweza kutumia changamoto ya maji taka katika eneo hilo kwa
kuigeuza kuwa fursa.
Amefafanua kuwa
wakihusisha wataalm wa mradi na viongozi wa mtaa wa vingnguti mji mpya,
walianza kuzungumza na kujadiliana na wakazi wa eneo hilo ili kuwezesha
kazi ya kuunganisha vyoo vyao katika mtandao wa mabomba ya kusafirisha
maji taka kuelekea kwenye mtambo wa kuzalisha gesi.
Amefafanua
kuwa chini ya mradi huo maji taka yote kutoka kutoka katika nyumba
zilizounganishwa kupitia mabomba yanakusanywa na kusafirishwa moja kwa
moja kwenye mtambo wa kuzalisha gesi.
Kwa
upande wake Mtaalam anayehusika na ujenzi, mafunzo na usimamizi wa mfumo
wa mradi huo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya
Uhandisi wa Mazingira Chuo Kikuu cha Ardhi Rukia Yange amesema mradi huo
ambao uko kwenye majaribio unalenga kuwapunguzia wananchi gharama za
uhifadhi wa maji taka kwa kuwapatia nishati ya gesi kwa gharama nafuu
itakayowasaidia kuondokana na matumizi ya mkaa.
Amesema
kwa kuanzia utawanufaisha watu 150 wa eneo hilo na kuongeza kuwa
kuanzia Desemba mwaka huu wataanza kuiweka gesi hiyo katika vifungashio
maalum vitakavyoanza kusambazwa majumbani mwao tayari kwa matumizi.
Amesema
gesi hiyo itamwezesha mwananchi kuitumia kwa kipindi cha mwezi mmoja na
kupunguza matumizi makubwa ya mkaa na uharibifu wa mazingira.
Aidha,
amesema gharama za mwananchi kuunganishwa katika mfumo huo inaanzia
shilingi 150,000/ kwa wale walio na vyoo vinavyoruhusu mfumo huo na
shilingi 700,000/= kwa mwananchi anayetaka kujengewa choo kipya katika
eneo lake la makazi gharama ambazo hulipwa kidogo kidogo kupitia
utaratibu wa mikopo nafuu ulioanzishwa.
Naye
Meneja Uhusiano wa DAWASA Bi. Neli Msuya akifafanua kuhusu mradi huo
amesema suala la ujenzi wa miundombinu ya kuchukualia maji taka na
matumizi ya gesi itakayozalishwa litakwenda sambamba na utoaji wa elimu
kwa wananchi hao juu ya matumizi na uhifadhi wa gesi hiyo.
Amefafanua
kuwa DAWASA inaendelea kuendesha mafunzo ya uzingatiaji wa usalama
katika matumizi ya gesi hiyo pamoja na suala la usafi, utunzaji na
ulinzi wa miundombinu ya kusafirishia maji taka iliyojengwa katika eneo
hilo ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu.
Ameeleza
kuwa mbali na mradi wa kuzalisha gesi DAWASCO kwa kushirikiana na wadau
wa matumizi ya Nishati endelevu na uhifadhi wa mazingira inatarajia
kuanzisha mradi wa kuzalisha mbolea itakayotokana na maji taka
yaliyohifadhiwa katika eneo hilo.
"DAWASA
tukishirikiana na wadau mbalimbali tuna mpango wa kuyatumia maji taka
haya yaliyohifadhiwa kuzalisha mbolea itakayotumiwa na wakulima katika
shughuli za kilimo,tunalenga kuibadilisha changamoto hii ya maji taka
kuwa fursa itakayowanufaisha wananchi badala ya kuwa kero kwao"
Amesisitiza.
Wakiuzungumzia mradi huo baadhi ya
wakazi wa mtaa wa mji mpya ambao vyoo vyao vimeunganishwa kwenye mfumo
wa kusafirishia maji Taka wamesema mradi huo ni ukombozi katika maisha
yao kwa kuwa umewapatia vyoo bora na kuwaondolea adha na gharama ya
uhifadhi wa maji taka waliyokuwa wakiipata hapo awali kutokana na
ujenzi holela wa makazi yao.
Wameongeza kuwa
mradi huo umewasaidia katika uhifadhi wa mazingira na kuondoa tatizo la
utiririshaji wa muda mrefu wa maji taka uliosababishwa na uwepo wa
mifumo mibovu ya vyoo vyao.
Wamesema kuwa
kutokana na uimarishaji wa mifumo ya kusafirisha maji uliofanywa na
DAWASA kwa kushirikiana na Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Wanafunzi
wa Chuo Kikuu cha Cambrige (CDI) na Taasisi ya utoaji wa mikopo ya
Bridge for Change wameondoa hofu waliyokuwa nayo ya kupata magonjwa ya
mlipuko ikiwemo kipindupindu na kutoas wito kwa wananchi katika maeneo
mengine kujiunga na mradi huo.
No comments:
Post a Comment