DAR-ES-SALAAM,
SEPTEMBA 14, 2015 – Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) utaadhimisha
miaka nane ya mafanikio katika kuongeza uwajibikaji kwa kuimarisha sekta ya
habari nchini Tanzania kupitia tukio ambalo litafanyika jijini Dar es salaam. Tukio
hilo litawaleta pamoja waandishi wa habari na wanataaluma wengine ambao wamewezeshwa
na misaada ya TMF, wafadhili, wadau wa sekta ya habari pamoja na taasisi za
kiraia na serikali.
Akiongea
kwenye mkutano na waandishi wa habari kutangaza tukio hilo, Mkurugenzi wa TMF,
Ernest Sungura alisema:
“Tarehe
22 Septemba, 2015 tutakuwa na tukio la madhimisho ambayo yatajumuisha maonyesho
kwa ajili ya waandishi wa habari waliowezeshwa na misaada ya TMF kuonyesha kazi
zao na jinsi gani zimechangia kuleta uwajibikaji na pia kuonyesha kazi ambazo
zimepandisha kiwango cha mijadala ya umma katika masuala husika hususani
utawala bora na haki za binadamu pamoja
na sherehe ya utoaji tuzo kwa waandishi waliowezeshwa na TMF na kazi zao kuweza
kuleta mabadiliko chanya. Vile vile kutakuwa na mjadala utakaohusisha wataalamu
wa habari na wanaharakati kutoka asasi za kiraia katika kujadili changamoto
mbalimbali kama vile kuwajengea uwezo wanahabari na pia kuweka mazingira
endelevu na uhuru wa habari. Sasa ni miaka nane tangu TMF ilipoanzishwa na
tumetoka mbali. Maadhimisho haya yatatupatia fursa ya kutafakari kwa pamoja
tulipotoka, mambo tuliyoyafanya na pia tutapeana changamoto kufikiri zaidi
jinsi ambavyo sekta ya habari nchini Tanzania inaweza kubadilishwa ili kukuza
uwajibikaji.”
Tangu
ilipoanzishwa mwaka 2008, TMF imetoa misaada na kuwawezesha waandishi wa habari
zaidi ya 570 na zaidi ya taasisi za habari 120. Katika kipindi hiki, TMF
imehusika na kuunga mkono jitihada za wadau wengine wa habari na asasi za
kiraia katika kukuza uhuru wa habari. Mtandao wa TMF umevuka jiji la Dar es
salaam na kufikia pembe zote za nchi na unawagusa viongozi waandamizi wa vyombo
vya habari pamoja na waandishi waliopo maeneo yote ya nchi.
Uchambuzi
wa TMF kuhusu taarifa mbalimbali zinazotolewa na vyombo vya habari unaonyesha
kwamba habari ambazo zimefadhiliwa na TMF zimegusa masuala ya vijijini kwa
kiwango kikubwa. Asilimia 82 ya misaada ya TMF uelekezwa ukilinganisha na
asilimia 25 iliyoelekezwa kwenye habari za mijini. Vilevile uchambuzi
umeonyesha kwamba taarifa zilizofadhiliwa na TMF huwa na ubora wa hali ya juu
ukilinganisha na taarifa za kawaida zinazoandikwa au kutangazwa na vyombo vya
habari nchini.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi wa TMF, maadhimisho hayo pia yatatumika kuzindua Tanzania
Media Foundation, taasisi mpya ambayo itachukua nafasi ya Tanzania Media Fund
ambao ni mradi ulioanzishwa na wafadhili.
“TMF mpya itakuwa ni mpango ulioanzishwa na Watanzania na kufanya kazi
katika misingi ile ile kama mradi wa TMF lakini itaelekeza nguvu zaidi katika
kuhakikisha yanakuwepo mazingira endelevu kwa ajili ya ukuaji wa TMF pamoja na
wanahabari wanaosaidiwa na TMF. Tutaanzisha upya mpango wa kuwezesha
upatikanaji wa habari ambazo zina maslahi makubwa ya taifa. Tutafanya kazi na
wazalishaji vipindi ili kuongeza habari za ndani ili kuvisaidia vituo vya
televisheni kutimiza wajibu wa kisheria kama ilivyoagizwa na TCRA ya kuwa na
vipindi asilimia 60 vinavyohusu masuala ya ndani. Tunataka kuhakikisha vituo
vya habari vinatoa habari za kukidhi mahitaji mbalimbali.”
"Tanzania Media Foundation itaanza kazi kwa kukutana na wadau
mbalimbali wa habari nchi nzima na itafanya nao kazi ili kutambua habari ambazo
zitaleta mabadiliko chanya katika jamii.”
No comments:
Post a Comment