Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Alphayo Kidata (katikati) akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu makusanyo ya mwezi machi mwaka huu.Wengine kutoka kushoto ni Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,Joctan Kyamuhanga na Kaimu Kamishna wa Kodi za ndani,Salum Yusuf.
Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) imekusanya na kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato mwezi Machi 2016 kwa asilimia 101.
Lengo hilo limevukwa baada
ya TRA kukusanya shilingi trilioni 1.31
kati ya lengo la shilingi trilioni 1.30.
Akizungumza na waandishi wa
habari Jijini Dar es salaam leo kuhusu mwenendo wa makusanyo ya mapato,
Kamishna Mkuu wa TRA Alphayo Kidata amesema ongezeko la makusanyo linatokana na
jitihada zinazofanyawa na TRA katika kuongeza kasi ya usimamizi wa ufuatiliaji
na ukadiriaji wa kodi kwa usahihi.
“Tumejitahidi kudhibiti
biashara za magendo katika maeneo ya Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi,
mipakani na maziwa yote, Alisema Kamishna Mkuu.
Amesema hadi kufikia Machi
2016, tayari TRA imekusanya shilingi Trilioni 9.89 sawa na asilimia 99
ya lengo la makusanyo ya shilingi trilioni 9.99
mwaka wa fedha 2015/2016.
Bw. Alphayo amewasisitiza wafanyabiashara
ambao hawajasajili biashara zao kufanya hivyo mara moja kupitia ofisi za TRA
zilizoko katika maeneo ya biashara zao na kwa wale wanaoshiriki vitendo vya
uingizaji bidhaa za magendo nchini amemewata kuacha mara moja kwani
vinaipotezea serikali mapato. “Wakikamatwa katika msako unaoendelea
watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutaifisha bidhaa hizo, kutozwa faini
pamoja na kifungo”, amesisitiza.
Kwa Wafanyabiashara ambao
wanastahili kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) Kamishna Mkuu amewataka
kujisajili katika ofisi yoyote ya TRA na wahakikishe wanataarifa muhimu ikiwemo
anuani inayotambulika na namba simu zinazofanya kazi.
“Natoa wito kwa
wafanyabiashara wote waliosajiliwa na VAT lakini hawatumii mashine za
kielektroniki za kodi (EFDs) watumie mashine hizo kwa mujibu wa sheria.
Wakibainika hawazitumii watachukuliwa hatua za kisheria kwani zoezi la ukaguzi
wa biashara linaendelea mtaa kwa mtaa katika mikoa yote. Aidha wananchi wanakumbushwa
kudai risiti za kodi kwa thamani halisi ya manunuzi kila wanapofanya manunuzi
au kupata huduma”, alisema Kamishna Mkuu na kuongeza kuwa wananchi wema na
wazalendo wenye taarifa za ukwepaji wa kodi wazifikishe TRA kwa usiri. TRA inawaahidi
donge nono ikiwa ni pamoja na kutunza siri za taarifa hizo. Vilevile
wanapoadaiwa rushwa au kutendewa isivyo wasisite kutoa taarifa mara moja.
Imetolewa na:
Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi
TRA- Makao makuu
No comments:
Post a Comment