Jacquiline
Mrisho-MAELEZO.
MOJA
kati ya sekta ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amezizungumza sana katika hotuba zake ni sekta ya Manunuzi ya Umma
ambayo ameonesha wasiwasi kuwa sekta hiyo ina mianya inayopoteza fedha za Umma.
Sheria
ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni zake imeweka bayana taratibu za
kufuata hadi Mkataba kukamilika katika kufanya manunuzi ya Umma.
Katika
hatua hiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali imepewa nguvu kupitia Kifungu cha 60
cha Sheria hiyo na Kanuni ya 59 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013.
Katika
kusisitiza hilo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Benno Sanga anasema kuwa msingi
mkubwa wa sheria hiyo ni ushindanishwaji wa wazabuni unaoweza kuiletea Serikali
thamani ya fedha.
“Kila
taasisi ya Serikali lazima ifuate Sheria ya Manunuzi ya Umma kwa manunuzi
mbalimbali ya vifaa vya ofisi, sheria hii imeweka utaratibu wa kuhakikisha fedha
iliyotumiwa inalingana na huduma inayopatikana”,anasema Sanga.
Hapo awali Kanuni ya
59 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013 ilikuwa inaelekeza kwamba mikataba
yote ya ununuzi wa umma ambayo thamani yake inafikia shilingi milioni hamsini
au zaidi ifanyiwe uhakiki na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya kusainiwa
lakini kwa sasa kanuni hizo zimerekebishwa kupitia Marekebisho ya Kanuni za
Ununuzi wa Umma za Mwaka 2016 na sasa mikataba ya ununuzi ambayo inatakiwa
kuhakikiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Kanuni 59(1)
ya Kanuni hizo ni ile yenye thamani ya kuanzia shilingi bilioni moja au zaidi
na mikataba ya ununuzi inayohusu ushindani wa zabuni ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Kanuni ya
59(2) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma, mkataba wowote wa aina hiyo ambao
haukufanyiwa uhakiki na Mwanasheria Mkuu utakuwa batili.
Aidha, Kanuni ya
59(5) inaelekeza kuwa Afisa Masuhuli anapaswa kuhakikisha kuwa ushauri wa
kisheria uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati akihakiki mkataba
husika umezingatiwa ipasavyo na kuingizwa katika rasimu ya mkataba.
Mwanasheria Mkuu wa
Serikali George Masaju amefafanua kuwa kwa mikataba ambayo iko chini ya thamani
ya shilingi bilioni moja inafanyiwa upekuzi na Afisa Sheria wa Taasisi ya
Manunuzi husika kama inavyoelezwa katika Kanuni ya 60(1).
”Hata
hivyo, kwa mujibu wa Kanuni ya 60(4) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma, Taasisi ya
Manunuzi haizuiwi kuomba ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa jambo
lolote linalohusu mkataba unaoweza kuhakikiwa na Afisa Sheria (Legal Officer)
wa taasisi husika”, anasema Masaju.
Divisheni ya mikataba ni moja ya ofisi
zilizoko chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayojumuisha
wanasheria wa taasisi ya manunuzi ya umma ambayo inashughulikia masuala yote ya
kuhakiki mikataba kwa makini ili kufahamu kama taratibu za manunuzi zimefuatwa pamoja na kutoa ushauri wa mikataba ya manunuzi ya
umma kwa taasisi mbalimbali za Serikali.
Divisheni hiyo ya
Mikataba ina jukumu la kutoa ushauri wa kisheria kwa taasisi za Serikali kwa
uadilifu na uweledi wa hali ya juu, kushiriki majadiliano kwa nia ya kuingia
makubaliano na nchi moja au zaidi ya moja.
Pia kushiriki katika
kazi mbalimbali za Serikali ambazo zinahitaji muongozo wa kisheria pamoja na
upekuzi wa mikataba ihusuyo Serikali ikiwemo ya hati za makubaliano, mikataba
ya upangaji, mikopo, madini, mafuta na gesi, ununuzi wa umeme, utekelezaji wa
miradi, mikataba itokanayo na zabuni.
Jukumu lingine ni kuangalia
ibara mbalimbali za mkataba kama zimewekwa sahihi ili kuondoa uwezekano wa
athari hasi kwa Serikali na kujiridhisha kama mikataba husika inakidhi au
kuzingatia maslahi ya Umma au Taifa.
Hata hivyo, “chochote
kizuri huwa hakikosi kasoro”, majukumu hayo yanaingiwa na changamoto nyingi kwa
kuwa Divisheni ya Mikataba iko katika Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali pekee.
Hivyo, mikataba hiyo
imekuwa ikipelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya kuhakikiwa, hatua ambayo imekuwa
ikisababisha wadau wa masuala hayo hasa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa,
Jiji na wengine walioko mikoani kusafiri na kupeleka mikataba Dar es Salaam kwa
ajili ya uhakiki. Mbali na kuongeza
gharama kwa halmashauri na wadau wengine, utaratibu huo unaweza kuchelewesha
mradi kuanza mapema.
Kutokana na
changamoto hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaona umuhimu wa
kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali waliopo katika ofisi zao za Mikoani ili
baadhi ya Mikataba iwe inahakikiwa na ofisi hizo.
Akifungua
semina ya mafunzo ya Mawakili wa Serikali yanayohusu Sheria ya Manunuzi ya
Umma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju anasema kuwa "Kutokana na
changamoto hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaona umuhimu wa
kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali wa Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali
zilizoko mikoani ili hatimaye baadhi ya mikataba kutoka kwa wadau walioko
wilayani na mikoani iwe inapelekwa katika Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali
zilizoko mikoani".
Masaju
anaongeza kuwa kutokana na kuongezeka kwa thamani ya mikataba inayohakikiwa na
Wanasheria wa Taasisi ya Manunuzi ni wazi kwamba wanasheria hao wanatakiwa
kujengewa uwezo kuhusu uhakiki wa mikataba kwani iwapo watashindwa kutekeleza
wajibu huo ipasavyo watawajibishwa kwa kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu
au kisheria.
Naye
Mkurugenzi Msaidizi wa Mikataba (Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali)
Bi.Monica Otaru anasema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia mawakili kufanya upekuzi
wa mikataba kwa makini na uhakika zaidi.
“Pamoja
na kuwa kazi ya kupekua mikataba ni sehemu ndogo ya kazi zetu lakini inachukua
muda mwingi, hivyo mafunzo haya yatawaandaa Mawakili wa Serikali walioko katika
Ofisi za Kanda kuweza kufanya upekuzi wa mikataba kwa umakini na uhakika
zaidi”,alisema Bi. Otaru.
Ili
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itekeleze wajibu huo wa kuhakiki mikataba
kwa ufanisi ipasavyo, Wizara, Taasisi na Idara za Serikali zinazopeleka
Mikataba katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali zinakumbushwa kuzingatia
mambo ya msingi.
Mambo
hayo ni masharti ya kifungu cha 22 cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, 2005, Kanuni ya 13(1) ya Kanuni za
Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya mwaka 2006
inayoelekeza namna ya kupata ushauri katika Ofisi hiyo kwa kuainisha maelezo
muhimu kuhusu mkataba husika.
Pia
kuandika barua ya kuiomba Ofisi kuhakiki mkataba husika ili Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali itoe ushauri wake ikiwa inaelewa vizuri yaliyomo
katika mkataba husika.
Wakati
wa mafunzo hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Divisheni ya Mikataba, Said
Kalunde anaelezea juu ya mambo muhimu ya kuzingatia katika kufanya upekuzi wa
mikataba ya ununuzi ikiwemo ya ujazaji wa fomu mbalimbali zinazotumika
katika uhakiki wa mikataba hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma.
“Ni
muhimu sana kwa wakili kujiridhisha kama taratibu za ujazaji wa fomu zimefuatwa
na fomu zimejazwa kwa usahihi, endapo wakili hatojiridhisha kwa kuhakiki fomu
hizo huenda akapatwa na matatizo makubwa ya kiutendaji”,alisema Kalunde.
“Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inapenda kuzikumbusha Wizara, Idara na Taasisi
za Serikali kuzingatia ipasavyo masharti ya kifungu cha 20(1) cha Sheria ya
Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali cha mwaka 2005
kinachoelezea kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia pale wizara na taasisi
zinapohitaji huduma za kisheria kutoka nje ya Ofisi ya Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.”anasema Kalunde.
Anafafanua
kuwa kifungu hicho kinaelekeza kuwa," Mkataba wa utoaji huduma ya kisheria
kwa Wizara au Taasisi ya Serikali uingiwe baada ya kupata kibali kwa maandishi
kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali".
No comments:
Post a Comment