Katika
jitihada za kuboresha huduma kwa walipakodi na kuzifikisha huduma hizo
kwa karibu zaidi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania ( TRA) Bw. Alphayo Kidata amezindua
ofisi
mpya ya TRA katika eneo la Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam Tarehe
26 Oktoba 2016 itakayotoa huduma zote za kikodi ikiwemo usajili na
uhakiki wa Namba za Utambulisho
wa Mlipakodi –TIN, Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani-VAT, Malipo
ya Kodi za Magari, Kodi zote za Mapato zikiwemo Kodi za Makampuni, Watu
Binafsi, Wafanyakazi (PAYE), Kuendeleza Ufundi Stadi - SDL, VAT, Ushuru
wa Stampu na huduma nyingine za kikodi.
Akizungumza
na walipakodi waliofika katika ofisi hiyo kupata huduma wakati wa
uzinduzi, Bw. Kidata aliwashukuru kwa mwitikio wao katika
zoezi la uhakiki wa taarifa za TIN ambao utaisaidia Mamlaka kupata
idadi sahihi ya walipakodi ili kuondoa walipakodi hewa ikiwa ni pamoja
na kuboresha huduma za ulipaji kodi.
“Zoezi hili litaongeza ufanisi katika suala zima la usimamizi na ukusanyaji kodi kwa kiwango cha juu”
Alisema Bw. Kidata
Kamishna
Mkuu wa TRA aliwataka walipakodi hao wanaoishi maeneo ya karibu na
ofisi hiyo mpya ya TRA iliyopo Kimara Mwisho kuendelea
kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma mbalimbali za kikodi ikiwemo
uhakiki wa taarifa zao TIN kabla ya tarehe ya mwisho wa zoezi hilo kwa
Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ni tarehe 30 Novemba 2016.
Aidha
Kamishna wa Kodi za Ndani TRA Bw. Elijah Mwandumbya alisema TRA
imejipanga kuhakikisha inaendelea kuboresha huduma zake na kuwafikia
walipakodi kwa ukaribu zaidi ili kuondoa usumbufu na kuokoa muda wa
upatikanaji wa huduma hizo.
“TRA kwa kuhakikisha walipakodi wanapata huduma iliyo bora imeanzisha vituo vingi vya kodi katika jiji la Dar es Salaam na nchi
nzima ili walipakodi wapate huduma stahiki na ya haki na kuiwezesha Serikali kupata mapato yake kwa mendeleo ya Taifa letu” Alisema Bw. Mwandubya.
No comments:
Post a Comment