Na Ismail
Ngayonga.Dar es Salaam
KATIKA kipindi cha miaka 20 wadau wa tasnia ya habari hapa nchini wamekuwa katika vuguvugu
la kudai mabadiliko ya mfumo wa sheria iliyopo sasa hasa ile ya magazeti ya
mwaka 1976, ambayo kwa kipindi kirefu imelalamikiwa kuwa inavibana vyombo vya
habari katika kutimiza wajibu wake kwa umma.
Wadau
hao wamekuwa wakiiona Sheria hiyo kuwa ni kandamizi kwa kumpa madaraka makubwa Waziri anayesimamia tasnia ya habari katika
utoaji wa adhabu dhidi ya chombo cha habari pamoja na tafsiri ya uchochezi.
Kwa
kuzingatia kilio cha wadau , ukuaji wa teknolojia na mabadiliko ya mfumo wa
maisha na mahitaji halisi ya jamii katika suala zima la upashanaji, ukusanyaji
na usambaji wa habari, Serikali iliona ipo haja kuanzishwa kwa chombo maalum
cha kusimamia maadili, maslahi, haki na wajibu wa vyombo vya habari.
Katika
kutekeleza ahadi yake kwa wadau wa habari nchini, Serikali iliwasilisha Bungeni
miswada miwili ya huduma ya habari na haki ya kupata habari, ambapo muswada wa
upakikanaji taarifa ulisomwa, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge ambapo
unasubiri idhini ya Rais ili kuwa sheria kamili.
Tarehe
Mosi Novemba mwaka huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ninatarajia
kuanza vikao vyake vya kawadia mjini Dodoma, ambapo Serikali itawasilisha
Bungeni miswada mbalimbali kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na Bunge hilo
ikiwa ni utekelezaji wa wajibu wa msingi wa chombo hicho, ambao ni kutunga
sheria.
Miongoni
mwa miswada inayotarajia kusomwa, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge ni pamoja
na Muswada wa sheria ya huduma ya habari, ambao
mjadala wake tayari umeteka hisia za watu wa kada mbalimbali za kijamii ikiwemo
wasomi, wadau wa habari na wananchi wa kawaida waliopo ndani na nje ya nchi.
Tangu
muswada huo uliposomwa Bungeni kwa mara ya kwanza tarehe 19 septemba mwaka huu,
wadau mbalimbali wa habari ikiwemo vyama vya taaluma ya habari, wamiliki,
wahariri na waandishi wa habari wamekuwa na misimamo na mitazamo tofauti kuhusu
muswada huo.
Akizungumzia
muswada huo Mkurugenzi wa Habari, Hassan Abbas anasema muswada huo umekusudia
kuiongezea heshima na hadhi tasnia ya habari, ili iweze kuwa taaluma kamili
kama zilizo fani za udaktari, uuguzi, ufamasia, sheria na nyinginezo.
“Fani
zote duniani zina chombo maalum cha usimamizi, kwa Tanzania pia tumeliona hilo,
wakati umefika sasa kwa wanahabari nao waunde bodi maalum ili kuifanya tasnia
ya habari kuwa taaluma yenye kuheshimika kwa jamii inayotuzungumza” alisema
Abbas
Anasema
kuwa maudhui ya muswada huo umezingatia mahitaji, haja, changamoto, na
mazingira ya kazi yanayomkabili mwandishi wa habari wa Tanzania katika
kutekeleza majukumu yake ya kazi za kila siku.
Anasema
jumla ya wadau 10 wa habari waliwasilisha maoni yao kwa Serikali, na asilimia
90 ya mapendekezo yao yameingizwa katika muswada huo.
Anazitaja
taasisi hizo ni pamoja na Baraza la Habari Tanzania, Jukwaa la Wahariri
Tanzania, Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari, Taasisi ya
Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN)
pamoja na vyama mbalimbali vya kutetea haki za kibanadamu nchini.
Kwa
mujibu wa Abbas alisema muswada huo umeweka mazingira yanayomtaka Mwajiri kutoa
Bima na Hifadhi ya Jamii kwa waajiriwa wake, ya kupitishwa na kusainiwa na Rais
Magufuli, waandishi wa habari watakuwa na kinga maalum ya matibabu pindi
wanapopata matatizo wakiwa kazini.
Anasema
kuwa hivi karibuni, waandishi wa habari wamekuwa wakikabiliwa na matatizo ya
kiafya ikiwemo kuugua na kifo, na hivyo wengi wao wakijikuta wakichangisha pesa
kwa ajili ya kugharamia huduma za matibabu.
Akizungumzia
kuhusu kifungu cha 55 cha muswada huo kinachozungumzia mamlaka ya Waziri, Abbas
anasema katika kipengele hicho madaraka ya Waziri yatajitokeza pale
panapokuwepo suala la dharura na linalohusu usalama wa taifa.
Anasema
kuwa yapo baadhi ya matukio yanayohitaji hatua za haraka kuchuliwa na Serikali,
ikiwemo uchapishaji na utangazaji wa habari zinazohamasisha uasi, uchochezi,
vurugu, mapigano ya kikoo na kadhalika ambapo Waziri mwenye dhamana ya
atawajibika kukifungia chombo hicho mara moja.
Anaongeza
kuwa muswada huo umetoa fursa kwa chombo na mwandishi wa habari kuikosoa
Serikali kuhusu sera, miongozo, matamko na maagizo mbalimbali ya Viongozi
ambayo yameshindwa kutekelezwa na Serikali.
Mkurugenzi
huyo anafafanua kuwa katika mikataba na sheria mbalimbali za kimataifa ikiwemo
kifungu cha 19 mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia, kimeainisha mipaka na
ukomo wa waandishi wa habari ikiwemo habari zinazohusu ulinzi na usalama wa
taifa, kashfa na maadili ya taifa.
Kwa
mujibu wa Abbas alitoa ufafanuzi kuhusu sheria hiyo kuwabana wamiliki na
watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa kuwataka kujisajili na suala hilo si la
kweli kwani litahusu vyombo vya habari vilivyo katika mfumo wa machapisho
ikiwemo magazeti na majarida.
“Sheria
itasimamia wote wa waandishi wa habari wa magazeti, redio na televisheni suala
la usimamizi wa maudhui ya vyombo vya habari vilivyopo katika mfumo wa
kieletroniki ikiwemo televisheni na redio wataendelea kusimamiwa na mamlaka ya
mawasiliano Tanzania (TCRA)” alisema Abbas.
Abbas
anasema kuwa muswada huo umekusudia kuanzishwa kwa Bodi huru ya habari
inayosimamia maadili na maslahi ya waandishi, ambapo itakuwa na wajumbe 7 na
wajumbe 4 wa Baraza hilo watatoka katika tansia ya habari akiwemo Mwenyekiti wa
bodi hiyo.
Aliyataka
majukumu ya bodi hiyo ni pamoja na kuandaa miongozo na miiko ya mwandishi wa
habari pamoja na kuandaa makongamano na mikutano ya mara itayowawezesha wadau
wa habari kukutana na kujadili changamoto mbalimbali zinaoikabili tansia ya
habari.
“Tasnia
ya habari ni nyeti sana, hivyo ni lazima iundiwe bodi yake, bila ya bodi
inaweza kuhatarisha usalama wa nchi” alisema Abbas.
Mwenyekiti
wa Chama cha Tanzania Labour Party, Augustino Mrema anasema muswada wa huduma
ya habari umekuja kwa wakati mwafaka kwani tasnia ya habari nchini wamekuwa
wakikabiliwa na kanzi kinzani mbalimbali ukosefu wa hifadhi ya jamii na bima ya
afya.
Akizungumzia
kuhusu Mamlaka ya Waziri yaliyoanishwa katika muswada huo, Mrema anasema
msimamizi wa sheria ya nchi yeyote duniani ni Serikali, ambapo hata hivyo
katika muswada huo Waziri amepewa mamlaka katika masuala ya dharura na usalama
wa taifa.
Mrema
anasema wadau wa habari ikiwemo vyama vya taaluma na wasomi kuacha malumbano
yanayoendelea katika mitandao ya kijamii na badala yake waungane na kuwa wamoja
ili muswada huo upitishwe na Bunge ili ipatikane sheria kamili inayowasaidia
waandishi wa habari katika kipindi cha miaka 50 hadi 100 ijayo.
Naye
Mhariri Mkuu wa kituo cha Redio Times, Zouhra Malisa anasema zipo taarifa
zilizoenea katika mitandao ya kijamii kuhusu kigezo na sifa ya mwanahabari
ambayo inamtaka mtumishi wa tasnia hiyo kuwa na shahada ya uandishi wa habari, na
hivyo kuibua woga kwa mustakabali wa tasnia ya habari nchini.
Anasema
kuwa kituo chake kimepanga kuwasilisha maoni kuhusu muswada huo, ambapo bodi ya
wakurugenzi na uhariri ya redio hiyo imepanga kuwasilisha mapendekezo yao
kuhusu muswada huo kabla ya kumalizika kwa muda uliotolewa na kamati ya kudumu
ya maendeleo ya jamii ya Bunge.
Aidha
Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Majira, Imma Mbughuni muswada huo ni mzuri,
hususani katika kipengele cha uanzishaji wa bodi ya ithibati itayohusika katika
utoaji wa vitambulisho vya wanahabari, ambavyo kwa kipindi kirefu vimekuwa
vikileta usumbufu mkubwa kwa waandishi wa habari.
Aidha
Mbughuni aliishauri Serikali kuusambaza huo muswada kwa wananchi wa kawaida kwa
kuwa itasaidia kupunguza minong’ono na malalamiko yanayotolewa na wadau wa
habari katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
No comments:
Post a Comment