Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Dar es Salaam.
KAMANDA
wa Polisi wa kikosi cha usalama Barabarani Mohammed Mpinga ametoa wito kwa
madereva wote ikiwemo madereva wa Serikali na Mashirika ya Umma kuzingatia
sheria za Usalama Barabarani.
Kamanda Mpinga ameyasema hayo leo jijini Dar es
salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa
kampeni ya kitaifa ya “Abiria paza sauti” inayotarajiwa kuzinduliwa tarehe
28 Novemba, mwaka huu.
Kamanda Mpinga alisema kumekuwa tabia ya baadhi ya
madereva hususani wa Serikali na mashirika ya umma ya kutofuata sheria za
usalama barabarani kwa kuendesha magari kwa mwendokasi, na kuwaonya kuwa sheria
ni msumeno na inapaswa kufuatwa na kila mtu.
“Kumekuwa na madereva hasa wa magari madogo
kusafiri kwenda maeneo mbalimbali ya nchi huku wakiwa hawana uzoefu wa
kuendesha umbali mrefu na hivyo kupelekea uvunjifu wa sheria za barabarani kwa
kuendesha kwa mwendokasi na kusababisha ajali” alifafanua Kamanda Mpinga.
Akifafanua zaidi Kamanda alisema uzoefu unaonyesha
kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka kumekuwa na ongezeko kubwa
la magari barabarani, na hivyo kuwataka wananchi kuzingatia sheria za
barabarani ili kuweza kupunguza ajali za barabarani.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya
Mabalozi wa Usalama Barabarani, Jackson Kalikumtima alisema lengo la kampeni ya
Paza Sauti ni kuhamasisha ushiriki kamilifu wa wananchi katika kukabiliana na
ajali kwa kuchukua hatua stahiki bila ya uwepo wa askari.
Pia alisema kuwa kampeni hiyo imelenga kubadili tabia na mtazamo wa
madereva kuhusu usalama barabarani ili waendeshe kwa kuzingatia sheria bila
shuruti na kubadili mtazamo wa wananchi kuhusu usalama barabarani ili watambue
kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja.
Naye Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani
nchini, (ASP), Deus Sokoni alisema mkakati wa kupunguza ajali barabarani katika
kampeni hiyo umelenga katika kutoa elimu
kwa jamii ili kuona suala la usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja na si
jukumu la Polisi pekee.
“hakuna asiyetumia barabara duniani, hatutaki ajali
tunataka kuishi salama, hivyo kila abiria anawajibu wa kutunza na kutii sheria
za barabarani “ aliongeza Mwanasheria huyo.
Mwenyekiti wa Chama
cha Kutetea Abiria Taifa (CHAKUA),
Hassan Mhanjama aliwataka abiria wote nchini hususani wanaotajaria kusafiri
mwishoni mwa mwaka kuwasiliana na Mamlaka ya Usafirishaji SUMATRA pindi
watakapopandishiwa nauli mbali na taratibu zilizopo.
No comments:
Post a Comment