Na Frank Shija, MAELEZO.
Serikali ya Awamu
ya Tano ndani ya mwaka mmoja imeanza mipango ya kuboresha usafiri wa reli ya
Kati kwa kuijenga kwa kiwango cha kimataifa yaani Standard Gauge. Usafiri huu
utaongeza fursa za kiuchumi kwani mazao ya chakula na biashara toka mikoa ya
Kigoma, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Singida kuelekea Dar es
Salaam yatasafirishwa kwa haraka.
Reli hii
itarahisisha pia usafiri wa abiria wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kati na
Magharibi. Usafiri wa treni kwa kiwango kikubwa huwa ni wa uhakika na wa
gharama nafuu. Hivyo ujenzi wa reli kwa Standard Gauge uteleta ukombozi mkubwa
wa kiuchumi kwa watu wa maeneo hayo na Taifa kwa ujumla.
Kwa kipindi
kirefu huduma ya usafiri wa treni kupitia Reli ya Kati (Central Line Railway)
imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma na maeneo ya Kanda ya ziwa
na nchi za jirani zikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo.
Historia
inaonesha kuwa Reli ya Kati kama inavyojulikana sasa ilijengwa kati ya mwaka
1905 hadi 1914 wakati huo ikiitwa Reli ya Tanganyika kwa kuwa ilikuwa ikielekea
Mkoani Kigoma ambako Ziwa Tanganyika linapatikana.
Kutokana na
umuhimu wake katika kukuza uchumi kupitia usafirishaji bidhaa na huduma
mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali
imeamua kuja na mpango kabambe wa kuifanyia maboresho miundombinu ya reli
hiyo ili iweze kwenda na wakati na kasi ya ukuaji wa uchumi.
Mpango huo
unahusisha ujenzi wa mtandao wa Reli mpya ya Kati katika Viwango vya Kimataifa
(Standard Gauge 80’) ili kuendana na kasi ya ongezeko la mizigo.
Msemaji wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Bw. William Budoya anaeleza kuwa gharama
iliyokaidiriwa kutumika kukamilisha mradi huo ni Dola za Kimarekani Bilioni 7.6
ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 16.
Fedha hizo
zitatumika kugharamia ujenzi wa Kilomita 2,561 za reli kwa kiwango cha
Kimataifa . Ili kufanikisha mradi huo Serikali imepata ufadhili kutoka Benki ya
Exim ya China ambayo imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu.
Aidha, katika
kuhakikisha kuwa ujenzi huo unafanikiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anakutana na kufanya mazungumzo na Rais wa
Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo
yao Rais wa benki hiyo anamuhakikishia Rais Dkt. John Magufuli kuwa Benki hiyo
iko tayari kutoa kiasi hicho cha fedha ili kufanikisha ujenzi wa kilometa 2,190
za reli. Pia anamuhakikishia Rais kuwa Benki hiyo itashirikiana na Tanzania
katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli
hiyo.
Akiuzungumzia
ujenzi wa Reli hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe
Magufuli anabainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuinua uchumi wa
Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo Uganda, Rwanda,
Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Anasema reli hiyo
mpya itakua tofauti na inayotumika sasa kutokana na uwezo wake wa
kuhimili usafirishaji wa mizigo mingi kwa kuwa inajengwa kwa kiwango cha
Kimataifa "Standard Gauge railway " na itaanzia Dar es Salaam Mpaka
Kigoma, kupitia Tabora, Mwanza,Isaka hadi Rusumo; Kaliua -Mpanda -Karema na
Uvinza -Musongati nchini Burundi.
Katika ufafanuzi
alioutoa hivi karibuni kuhusu ujenzi wa reli hiyo wakati wa Mkutano Mkuu Maalum
wa Chama cha Mapinduzi mjini Dodoma hivi karibuni, Rais John Pombe Magufuli
alisema tayari mchakato wa ujenzi wa reli hiyo umeanza kwa kutangaza zabuni ili
kumpata mkandarasi atakaye jenga Reli hiyo.
Anasema sambamba na kazi hiyo Serikali itakarabati
matawi ya reli ya kati sehemu ya Kaliua-Mpanda ili kuboresha ufanisi wake, kwa
kutenga Sh. bilioni 5.5 za ajili ya usanifu.
Aidha, Mpango wa
Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano uliowasilishwa bungeni Dodoma na Waziri wa
Fedha na Mipango ,Dk. Philip Mpango unaeleza kuwa Serikali imejipanga kufanya
usanifu na ujenzi wa madaraja 16 kati ya 28 yaliyochakaa kati ya Dar es Salaam
na Tabora.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango, Dkt. Servaciaus Likwelile akizungumza mara baada ya utiaji saini wa
makubaliano wa ujenzi wa reli hiyo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Naibu
Meneja Mikopo Nafuu wa Benki ya Exim ya China Bw. Zhu Ying anasema kuwa Dola za
Kimarekani bilioni 7.6 ambazo ni sawa na Shilingi Trilioni 16 zitatumika
kutekeleza mradi huo.
Dkt. Likwelile anasema hatua hiyo
inawezesha kuanza kwa kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu na uundwaji wa timu za
pamoja kuanza kuainisha mahitaji halisi ya ujenzi wa mradi huo.
Anasema mradi huu
umekuja wakati muafaka kutokana na kwamba reli iliyopo sasa ambayo ni ya
Kiwango cha "meter gauge” haina uwezo mkubwa katika ubebaji wake wa
mizigo, hata baada ya kufanyiwa ukarabati.
Kwa mwaka ni tani
Milioni 5 za mizigo ndizo zinaweza kupitishwa na reli ya sasa, ambazo haziwezi
kukabili mahitaji ya mizigo ya Kanda hii ambayo itafikia tani Milioni 30
ifikapo mwaka 2025.
Kutokana na
uhitaji huo wa kukabiliana na uongezaji wa mizigo kwa kujenga uwezo wa
kuihudumia kwa kuwa na reli ambayo pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba mizigo
hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi na kwa starehe lakini pia
kwa kasi ya spidi ya wastani wa kilometa 100 kwa saa hivyo kuwezesha abiria
kufika haraka zaidi sehemu wanazokwenda.
Pia wakati wa
ujenzi wa reli hiyo watanzania takribani 300,000 watapata ajira kutokana na
kushiriki katika ujenzi wa reli hiyo.
No comments:
Post a Comment