Meneja wa Idara ya Pato la Taifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Daniel Masolwa (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yatakayofanyika kesho Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Kulia ni Ofisa Habari wa Idara Habari Maelezo, Beatrice Lyimo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale.
WAZIRI wa Fedha Dk. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yatakayofanyika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM)
Maadhimisho hayo yatafanyika kesho kuanzia saa tatu asubuhi ambapo wadau mbalimbali wa masuala ya takwimu na wananchi watahudhuria.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi Meneja wa Idara ya Pato la Taifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Daniel Masolwa alisema maadhimisho hayo ni muhimu sana na kuwa kauli mbiu yake ya mwaka huu ni " Kuimarisha Takwimu za Kiuchumi kwa Mtangamano wa Kikanda, Mabadiliko ya Miundo na Maendeleo Endelevu"
Masolwa alisema lengo kuu la kuadhimisha siku hiyo ni kuongeza uelewa mpana kwa watumiaji wote wa Takwimu Afrika kuhusu umuhimu wa takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo katika sekta zote za kijamii na kiuchumi katika Bara la Afrika.
Aidha alisema ni siku ambayo hutoa fursa kwa nchi kutathmini na kufuatilia malengo yaliyofikiwa katika Mipango ya Maendeleo ya ndani na nje ya Nchi.
Alisema Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika huwa yanaandaliwa na kauli mbiu mbalimbali kila mwaka zinahusiana na umuhimu wa takwimu katika kupanga maendeleo na kutunga sera katika Bara la Afrika.
Masolwa alisema umuhimu wa kuboresha na kuimarisha takwimu za kiuchumi na zenye ubora kwa utangamano wa kikanda barani Afrika utasaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kufanikisha malengo endelevu, Agenda 2063 ya Afrika na mipango ya kitaifa ya kukuza uchumi.
No comments:
Post a Comment