Na. Lilian Lundo –
MAELEZO.
Askofu wa Good News for All Ministry Dkt. Charles Gadi kwa niaba ya dini na madhehebu mbalimbali
hapa nchini wamempongeza Rais Dk. John
Magufuli kwa kumteua Kamishna wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya.
Dk. Gadi ametoa pongezi hizo,
Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na vyombo vya habari katika ukumbi wa
Idara ya Habari (MAELEZO).
“Tunamshukuru Mungu kwa kumuinua Rais
ambaye ameonyesha nia na kuwa mstari wa mbele
kupigana na biashara hiyo haramu, ni ukweli usiopingika kwamba tatizo la
dawa ya kulevya ni kubwa na lenye
madhara makubwa sana kwa watanzania
wengi haswa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa,” alifafanua Dk. Gadi.
Aliendelea kwa kusema kuwa, Vijana
wengi wamepoteza maisha , kuharibika akili, kupata magonjwa ya kuambukiza, kupoteza malengo ya kimaisha kwa sababu ya dawa hizo.
Vile vile dawa hizo zimeleta fedheha kwa Taifa kutokana na Vijana wengi wa
Kitanzania kuwepo katika magereza mbalimbali Duniani huku wengine wakisubiri adhabu
ya kunyongwa.
Aidha amempongeza Rais Dk. Magufuli
kwa kuimarisha Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kumteua Kamishna ambaye atasimamia Mamlaka
hiyo na anaamini kwamba kwa neema ya Mungu ataweza kumsaidia kikamilifu Rais Magufuli katika kutimiza azma yake ya
kukomesha biashara hiyo.
Wakati huo huo, Dkt. Gadi amempongeza
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuianzisha vita hiyo dhidi ya matumizi ya dawa
kulevya katika mkoa wa Dar es Salaam. Vile vile amewapongeza waandishi wa
habari na vyombo mbalimbali vya habari kwa kutoa habari zinazosaidia katika
upambanaji wa biashara hiyo.
Dkt. Gadi amewataka viongozi wa Dini
kuungana bega kwa bega na Rais Magufuli kwa kuendelea kutoa maadili kwa vijana
ili kuepukana na uovu wa dawa za kulevya nchini.
Askofu wa Good News for All Ministry Dk. Charles
Gadi (wa tatu kutoka kushoto) pamoja na Maaskofu wa Madhehebu Mbalimbali
wakimuombea Rais Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya mkutano na waandishi wa
habari (hawapo pichani) katika ukumbi wa Idara ya Habari -MAELEZO, Jijini
Dar es Salaam.
Maaskofu wa Madhehebu mbalimbali wakimuombea Rais
Dk. John Magufuli mara baada ya mkutano na waandishi wa habari (hawapo
pichani) katika ukumbi wa Idara ya Habari -MAELEZO.
Maaskofu wa Madhehebu mbalimbali nchini
wakiongozwa na Askofu wa Good News for All Ministry Dk. Charles Gadi (wa tatu kutoka kushoto)
wakiombea Bendera ya Tanzania ili Amani iendelee kutawala.
No comments:
Post a Comment