NA HASSAN SILAYO-MAELEZO.
Tatizo la ongezeko la idadi ya vijana
na watu wazima waliokosa elimu ya sekondari ni kubwa sio tu hapa Tanzania bali
ni kwa nchi zote za kusini mwa jangwa la sahara, Kwa mfano, kwa takwimu za sensa
ya mwaka 2012, Tanzania ina jumla ya vijana wa umri wa miaka 7-17 milioni 3.5 ambao
wapo nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Hii hufanya vijana milioni 2.5 kuhitaji
elimu ya sekondari na wengine milioni 1 kuhitaji elimu ya msingi na ukweli ni
kwamba vijana wanaomaliza elimu ya msingi na kupata alama za ufaulu chini ya
100 (kati ya 250) wamekuwa wakiachwa bila kwenda sekondari katika Mikoa
mbalimbali isipokuwa wale ambao wazazi/walezi wao wanauwezo wa kuwapeleka
kwenye shule za sekondari za binafsi ambazo gharama zake ni za juu.
Takwimu za sensa ya mwaka 2012
zinaonesha kuwa kufikia mwaka 2015 idadi ya vijana walio nje ya shule
itaongezeka kufikia milioni 5.
Ili
kukabiliana na tatizo hili, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ilianzisha programu
ya elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi mwaka 1992 ili kutoa fursa ya elimu ya
sekondari kwa vijana na watu wazima waliokosa nafasi ya kuendelea na elimu ya
sekondari kwa sababu mbalimbali.
akiongea
kuhusu programu hiyo Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima
Dkt.Kassim Nihuki alisema Programu inawalenga wanafunzi waliomaliza darasa la
saba ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari na wale ambao
kwa sababu moja au nyingine hawakumaliza elimu ya sekondari na wanataka
kumaliza elimu hiyo.
Dkt.
Nihuki aliongeza kuwa programu hii pia inawalenga wanafunzi ambao wamemaliza
masomo ya MEMKWA (mpango wa elimu ya msingi kwa walioikosa) na wale wamemaliza
masomo ya sekondari lakini hawakufanya vizuri na wangependa kurudia mtihani wa
Taifa wa kidato cha nne pamoja na wafanyakazi wa serikali na sekta binafsi
ambao hawana elimu ya sekondari na wanatakiwa wawe na kiwango hicho cha elimu.
Dkt
Nihuki anasema kuwa masomo katika programu hii yanatolewa katika hatua tatu
kubwa ikiwa hatua ya kwanza inabeba
masomo ya kidato cha kwanza na chapili huku hatua ya tatu ikibeba masomo ya
kidato cha tatu na nne na hatua ya tatu
inabeba masomo ya kidato cha tano na sita.
Naye
Mkuu wa Idara ya Elimu Msafa Bw. Baraka Kionywaki amesema kuwa Katika hatua ya
I, mlengwa anasoma kwa kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuwa na sifa ya kufanya
mtihani wa maarifa (yaani “Qualifying
test”).
Bw. Kionywaki
aliongeza kuwa jumla ya masomo 7 ya lazima yanayotolewa katika hatua hii ambayo
ni Historia, Jiografia, Kiingereza, Kiswahili, Hisabati, Biolojia na Uraia
(Civics). Aidha, mlengwa anaweza kuchagua masomo ya ziada ya sayansi au
biashara kwa kadri atakavyoona inafaa.
Mlengwa wa hatua ya II anasoma kwa kipindi cha mwaka mwingine mmoja na
hivyo kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne unaoandaliwa na Baraza
la Mitihani la Taifa (NECTA).
Katika
hatua ya tatu mlengwa atasoma kwa kipindi cha mwaka mwingine mmoja na hivyo
kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha sita unaoandaliwa na NECTA. Ambapo
katika hatua hii, masomo yanatolewa katika tahasusi (“combinations”) za HGL (Historia, Jiografia na Lugha), HKL
(Historia, Kiswahili na Lugha), HGK (Historia, Jiografia na Kiswahili) na HGE
(Historia, Jiografia na Uchumi). Hata hivyo mlengwa katika kila hatua anaweza
kusoma kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi pale atakapokuwa amejiandaa kiasi cha
kutosha kufanya mtihani wa maarifa au ule wa NECTA.
Katika hatua zote, masomo
yanatolewa kupitia mafunzo ya ana kwa ana ya jioni (evening programme) kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 12 jioni pamoja
na kujisomea moduli na vitabu na matumizi ya teknolojia za kujifunzia kama vile
“CDs” na elimu mtandao (e-learning) yakiwemo
machapisho huria ya kielimu (open
educational resources).
Programu hii
ambayo inaendeshwa katika majengo ya shule
za msingi na sekondari za serikali 83 na shule za wadau mbalimbali 337 nchini zimewanufaisha vijana na watu
wazima 95,140 (wanawake 61049 na wanaume 44893) katika mikoa mbalimbali kwa kipindi cha tangu
mwaka 2010 hadi 2016.
No comments:
Post a Comment