Mkutano
Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
unatarajiwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu baada ya ule wa Dharura wa
marekebisho ya Katiba ulipangwa kufanyika Julai 13 mwaka huu.
Tarehe
hizo zimepangwa na kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya TFF
kilichofanyika leo (Mei 9 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya
uenyekiti wa Rais wake Leodegar Tenga ambacho kupokea rasmi maagizo ya
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na kupanga utekelezaji
wake.
“Kamati
ya Utendaji ya TFF imepokea rasmi barua ya FIFA na kupanga utekelezaji
wake. Tumepokea maagizo ya FIFA yanayotuelekeza cha kufanya, si TFF wala
mtu mwingine yeyote anayeweza kuongeza jambo lingine.
“Maagizo
ni undeni Kamati ya Maadili, Kamati ya Rufani ya Maadili, fanyeni
marekebisho ya Katiba, anzeni tena uchaguzi, waliokuwepo na wengine
wapya waruhusiwe. Tumejitahidi kuhakikisha uchaguzi uwe kabla ya Oktoba
30 mwaka huu kama FIFA walivyotuagiza,” amesema Rais Tenga wakati
akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema
kazi kubwa itakuwa ni kutayarisha kanuni hizo, kwani Kamati za Maadili
lazima ziwe na kanuni zake na kuhakikisha kuwa hakuna mgongano kati ya
Kanuni za Nidhamu na Kanuni za Maadili.
Pia
Rais Tenga amesema kuna kazi ya kuangalia jinsi zitakavyoingia katika
uchaguzi ambapo maana yake muda wa mchakato wa uchaguzi utakuwa zaidi ya
siku 40 za sasa, hivyo mabadiliko hayo yatagusa vilevile Kanuni za
Uchaguzi.
Kwa
mujibu wa ratiba ya utekelezaji, rasmu ya mwanzo ya Kanuni hizo
inatakiwa iwe imetoka kufikia Mei 30 mwaka huu ambapo itapelekwa FIFA
kwa ajili ya kupata mawazo yao kabla ya kuendelea na hatua inayofuata.
Juni
15 mwaka huu Kamati ya Utendaji ya TFF itakutana kupokea mapendekezo
hayo ambapo baada ya kuyapitisha itayapeleka tena FIFA. Taarifa (notice)
ya Mkutano Mkuu wa Dharura ambayo kikatiba ni siku 30 itatolewa Juni 12
au 13 mwaka huu.
Baada
ya Mkutano Mkuu wa Dharura wa marekebisho ya Katiba, Kamati ya Utendaji
itakutana kati ya Julai 14 na 15 mwaka huu kuunda Kamati ya Maadili na
Kamati ya Rufani ya Maadili ili kuruhusu mchakato wa uchaguzi uanze.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment