Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea
kwa mfadhaiko, mshituko na huzuni kubwa taarifa za shambulio la mlipuko
lililotokea katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mjini
Arusha jioni ya leo, Jumamosi, Juni 15, 2013, tukio ambalo limesababisha vifo
vya watu wawili na majeruhi ya Watanzania kadhaa.
Aidha,
Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa jamaa na ndugu wa wafiwa wote na
pia ametuma pole nyingi kwa majeruhi ambao wameumizwa na kujeruhiwa katika
tukio hilo ovu na katili.
Vile
vile, Rais Kikwete amewatumia salamu za pole viongozi wa CHADEMA kufuatia tukio
hilo la woga mkubwa na pia kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua
hatua stahiki za kuchunguza kwa haraka, kubaini, kuwakamata na kuwafikisha
mbele ya sheria wote waliohusika na tukio hilo, wawe watu wa ndani ya nchi ama
nje ya nchi.
Katika
salamu zake za rambirambi na za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa
Magesa Mulongo, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mfadhaiko, mshituko na
huzuni kubwa shambulio la mlipuko lililotokea katika mkutano wa CHADEMA mjini
Arusha jioni ya leo, tukio ambalo limesababisha vifo na majeruhi ya Watanzania
wenzetu.”
Amesema
Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Magesa Mulongo
salamu zangu za rambirambi kufuatia vifo na pole nyingi kutokana na majeruhi
katika tukio hilo na naomba kupitia kwako unifikishie salamu zangu za
rambirambi kwa jamaa na ndugu wa wafiwa na pole nyingi sana kwa majeruhi.”
“Kadhalika
naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA
kutokana na tukio hilo. Naomba uwajulishe kuwa uchungu wao ni uchungu wetu sote
na msiba wao ni msiba wetu pia. Nataka wajue kuwa tupo pamoja nao katika
kipindi hiki kigumu na cha majonzi na huzuni mkubwa,” amesema Mheshimiwa Rais
Kikwete.
Rais
Kikwete amemwambia Mkuu wa Mkoa wa Arusha: “Kadhalika, nimeviagiza vyombo vya
ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka kuwasaka wahusika, kuwakamata na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Aidha, nawataka viongozi wa Serikali
ngazi ya kitaifa, Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Arusha mjini kuhakikisha kuwa
majeruhi wote wanapata matibabu ya haraka na huduma za tibabu stahiki.”
Aidha,
Rais Kikwete ametoa wito maalum kwa wananchi akisema: “Kwa wananchi wenzangu,
Watanzania wenzangu, napenda kutoa wito wa kuviachia vyombo vya ulinzi na
usalama kufanya kazi yao vizuri ili tuweze kuwabaini waovu waliofanya kitendo
hiki.”
“
Natambua kuwa yatakuwepo maneno mengi na hisia mbali mbali zitakazojaribu
kulielezea tukio hilio ovu na katili kwa njia mbali mbali. Nawasihi tujiepushe
na kuchukua dhana na hisia zetu au maneno ya watu wengine kuwa ni ukweli wa
tukio hili. Tujipe nafasi ya kutafakari vizuri na kufanya uamuzi ulio bora.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Mimi siamini kuwa Watanzania au wafuasi wa vyama vya siasa
wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya unyama wa aina hii. Naamini kuwa
hiki ni kitendo cha mtu ama watu wasioitakia mema nchi yetu, watu ambao
wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki miongoni mwa raia ama makundi ya
raia, ili nchi yetu iingie kwenye machafuko makubwa.”
“Ndugu
zangu, Watanzania wenzangu, naomba tuzinduke, ili tusiwape nafasi watu
hawa waovu ya kuweza kutimiza malengo yao ya kuvuruga amani na utulivu wa nchi
yetu kwa kuleta mifarakano baina yetu. Mungu Ibariki Tanzania, Munfu Ibariki
Afrika.”
No comments:
Post a Comment