Na Anna Nkinda – New York
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya Malengo ya Maendeleo
ya Milinia ya mwaka 2013 kwa wanawake na Shirika la Voices of African
Mothers (VAM) la nchini Marekani kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya
kusaidia jamii wakiwemo wanawake na watoto.
Sherehe ya kukabidhi tuzo hizo zilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) amekabidiwa tuzo hiyo kutokana na uongozi wake madhubuti,
mafanikio na mchango wake na kujitoa kwake kuwasaidia wanawake na watoto
wa Tanzania.
Akikabidhi tuzo hizo Nana – Fosu Randall ambaye ni Rais na mwanzilishi wa shirika hilo alisema kuwa tathimini ilitofanyika kwa mwaka 2012 juu ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia wametambua kwamba malengo matatu yamefikiwa nchini Tanzania kabla ya muda uliowekwa wa kikomo wa mwaka 2015.
Alisema
kuwa wake wa Marais wa Afrika wanamajukumu mbalimbali katika nchi zao
ili kufikia Malengo hayo, Taasisi ya VAM imekuwa ikifanya tathimini juu
ya hatua zilizofikiwa na Taasisi za wake wa Marais kupitia taarifa za
mwaka na zingine zinazowasilishwa.
“Wanawake hawa wanastahili kutuzwa kwani
wamefanya kazi kubwa pamoja na kufanya shughuli zao katika mazingira
yenye changamoto nyingi ukilinganisha na wenzao katika nchi zingine.
Hafla
ya tuzo hizi siyo tu inasherehekea mafanikio ya wake wa marais wa
Afrika bali pia inawahamasisha na kuwatia moyo wakati huu ambapo mwaka
2015 unakaribia”, alisema .
Alimalizia kwa kusema kuwa mara nyingi vyombo vya habari vimekuwa vikiandika habari zisizokuwa
sahihi kutokana na kazi zinazofanywa na wake wa marais lakini vinasahau
kuandika mambo mazuri na kazi kubwa wanayoifanya ya kuwasaidia wananchi
na kuviomba vyombo hivyo kubadilika na kuthamini kazi kubwa wanayoifanya.
Akiongea
mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Mama Kikwete alishukuru kwa tuzo
aliyopewa na kusema kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimepiga hatua
kubwa sana katika kufikia malengo ya milinia kwani vifo vya watoto
vimepungua kwa asilimia 45 na 49 kwa watoto wachanga.
Alisema
kuwa haya ni mafanikio makubwa sana japokuwa lengo ni kuondoa kabisa
vifo ambavyo vinatokana na sababu ambazo zinazuilika na
katika malengo mengine maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) yanaendelea
kupungua kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka 2004 hadi asilimia 5.1 kwa mwaka
2011.
Mama
Kikwete alisema, “Elimu ya msingi inatolewa bure kwa watoto wote walio
na umri unaostahili na hatua kubwa imepigwa katika kupunguza ugonjwa wa
maralia na vifo vya akina mama vinavyotokana na tatizo la uzazi”
Kwa
upande wa harakati za kumkomboa mtoto wa kike alisema kuwa ni lazima
ziendelee na zizingatie changamoto mpya za mazingira mapya kwani
unapompatia elimu unampunguzia changamoto za ujinsia na kumpatia huduma
ya afya ikiwemo uzazi wa mpango, unamuwezesha kushiriki zaidi shughuli
za maendeleo ya kiuchumi, unasaidia familia yake na jamii kuweza
kuendelea.
Kwa
upande wake Dk. Judy Kuriansky ambaye ni mwakilishi wa Asasi zisizo za
Kiserikali zilizo chini ya UN alisema kuwa wake wa marais wanafanya kazi
kubwa ya kuisaidia jamii hivyo basi ni jukumu la kila mmoja kuwaunga
mkono na kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kutimiza malengo ya
maendeleo ya milinia.
Dk.
Kuriansky alisema kuwa ili kufikia malengo ya milinia inatakiwa
kuimarisha miundombinu iliyopo jambo ambalo litasababisha kuifikia jamii
kwa ukaribu zaidi na kuweza kutatua changamoto zinazowakabili.
Tuzo
hizo zimetolewa kwa mara ya kwanza na shirika hilo kwa kushirikiana na
Taasisi ya The reed for Hope (RFHF) na Bethesda Counsel kwa wake wa
marais wa Afrika akiwemo Mke wa Rais wa Burundi Mama Dk. Denice
Nkurunziza, Mke wa Rais wa Equatorial Guinea Mama Constancia Mangue de
Obiang na Mke wa Rais wa Mali Mama Mintou Doucoure Epse Traore.
No comments:
Post a Comment