Moto uliowashwa na baadhi ya watu
wakifunga barabara baada ya kutawanywa na Polisi kwa mabomu ya machozi
katika viwanja vya SOWETO vilivyopo jijini hapa, barabara Iiliyopo eneo
la Kaloleni. (Picha zote na Ferdinand Shayo)
Moto ukiwaka katikati ya barabara wakati wa vurugu zilizotokea katika viwanja vya SOWETO mjini Arusha.
Wanafunzi
wa shule wakijiziba na nguo na kunawa uso baada ya kudhuriwa na mabomu
ya machozi yaliyopigwa leo na Polisi waliokuwa wakitawanya maelfu ya watu waliokuwa kwenye mkutano katika viwanja vya SOWETO.
Baadhi ya
watu wakifunga barabara baada ya kutawanywa na Polisi kwa mabomu ya
machozi katika viwanja vya SOWETO vilivyopo jijini hapa, Barabara Kuu
inayopitisha magari ya mikoani eneo la Kimahama.
TANZANIA,ARUSHA
MBUNGE wa Mbulu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Mustafa Akoonay, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu
Lissu, viongozi wengine wa Chadema na wafuasi kadhaa wa chama hicho
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Arusha kwa mahojiano kufuatia vurugu
zilizoibuka katika mkutano wa hadhara.
Akizungumza na TANZANIA LIVE BLOG, kutoka jijini Arusha, Kamanda wa Polisi mkoa huo, Liberatus
Sabas alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao waandamizi wa Chadema na wafuasi
wa chama hicho muda mfupi baada ya mkutano wa dharura wa chama hicho katika
uwanjwa wa Soweto.
Jeshi la Polisi lilivunja mkutano huo kwa kutumia gesi ya
machozi yaliyorindima kwa zaidi ya saa mbili kutawanya wafuasi wa chama hicho
uwanjani hapo, kutokana viongozi hao kutumia nafasi ya maombolezo kuendesha
mkutano hadhara ambao haukuwa na kibali.
Watu kadhaa wanadaiwa
kupoteza maisha katika tafrani hiyo, huku wengine wakijeruhiwa na kufikishwa
hospitali mbalimbali jijini humo, ikiwemo Hospitali ya Seliani kwa matibabu baada
ya kuumizwa na askari, huku wengine wakipata mshtuko iliyosababishwa na mlipuko
wa mabomu ya machozi.
Wakiwa ndani ya magari madogo, askari polisi walilipua mabomu
hayo maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha hali iliyowalazimu wafanyabiashara
jijini humo kufunga biashara zao na kukimbia wakihofia kuvamiwa na wakazi
waliokuwa wakikimbia hovyo kunusuru maisha yao.
Hali ya usafiri
iligeuka adha nyingine kwa wakazi wa jiji la Arusha, baada ya daladala
kushindwa kutoa huduma hiyo, zikihofia mabomu yaliyokuwa yakirushwa na askari,
huku barabara zikifungwa baada ya wafuasi wa CHADEMA kuchoma matairi barabarani.
Tafrani hiyo kwa
namna moja iliwaathiri hata wanahabari, ambao walijikuta wakipata adha ya
ulipuliwaji wa mabomu hayo na kulazimika kujificha katika magofu ya nyumba za
AICC zilizoko karibu na uwanja wa Soweto kwa zaidi ya masaa mawili.
Aidha, mapema Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda, alikiri
kuwa uchunguzi wa haraka umebaini kuwa bomu lililotumika kulipua katika mkutano
wa Chadema juzi limetengezwa China, na aina hiyo ya mabomu yanamilikiwa na
vyombo vya dola, hasa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
No comments:
Post a Comment