KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Friday, July 19, 2013

MAMA SALMA KIKWETE AWATAKA WANAWAKE KUTOBAGUANA KUTOKANA NA TOFAUTI ZAO ZA VYAMA VYA SIASA.

Na Anna Nkinda – Maelezo
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wanawake wa dini zote nchini kutokubaguana kutokana na  itikadi zao za  vyama vya siasa bali wawe mstari wa mbele kuhubiri amani na upendo.
Mama Kikwete aliyasema hayo jana wakati akiwafutarisha  wanawake wa dini mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete alisema kuwa ukosefu wa amani ukitokea katika nchi wanawake na watoto ndiyo wahanga wakubwa  hivyo basi wasikubali  watu kuwadanganya bali wawe na msimamo  na  umoja ili waweze kuilinda amani ambayo ndiyo silaha pekee ya kuwaletea ukombozi  iliyoasisiwa na wazee wa nchi yao.
“Ninawashukuru kwa kuacha shughuli zenu na kuitikia wito wangu wa kuja na kufuturu pamoja nami, nawatakia mfungo mwema nini nyote mnaofunga ili Mwenyezi Mungu awakubalie heri zenu nanyi msiofunga Mwenyezi Munguawabariki katika maisha yenu ya kila siku”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuia ya  Wanawake wa Kiislamu Tanzania Taifa  (BAKWATA) Shamim Khan alimshukuru Mama Kikwete kwa upendo wake wa kuwaalika wanawake hao kupata futari ya pamoja. 
Mama Khan alisema kuwa kukutana kwao  kumewafanya wajifunze  kuwa wakitaka amani ni lazima washirikiane bila ya kujali rangi, dini na kabila kwani wanawake wote wanamatatizo yanayofanana ambayo wanaweza kuyatatua kwa pamoja bila ya kuangalia  kuwa huyu ni mkristo au muislamu na  wakikaa pamoja amani inapatikana.
Naye  Olive Lwema ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake wakristo Tanzania alisema kuwa aliposikia wamepata mwaliko huo alifurahi sana kwasababu wanapokutana wanawake ambao ni wazazi wa watoto wa taifa, wake wa waume wanaoongoza nchi hakuna jambo litakaloharibika na ameshuhudia kwa kuona nyuso za ushirikiano na upendo baina yao.
Mama Lwema aliwaomba wanawake wanaofunga  kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wajitoe kufunga kwao kwa ajili ya maombi maalum ya kuombea amani na watoto kwani hivi sasa vijana wengi wanaomaliza vyuo  hawana ajira, shule haziendi sawa na wanaopata machungu ya haya yote ni wanawake.

No comments: