Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa,
Adoh Mapunda akizungumza na
waandishi jijini Dar es Salaam juzi,
kuhusu maendeleo ya wilaya hiyo na faida
wanayoipata kutokana na gesi ya Songosongo. Katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya,
Mohamed Mtopa na Diwani wa Kata
ya Karanjeranje, Ally Mtotela.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Dar es
salaam
Uongozi wa Halmashauri
ya wilaya ya Kilwa umesema kuwa utahakikisha rasilimali zote zinazopatikana katika wilaya
hiyo ikiwa ni pamoja na gesi asilia zinatumika kuleta maendeleo na kuboresha
maisha ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa
leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Bw. Adoh Mapunda wakati akitoa
ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa huduma za jamii kwa
kutumia rasilimali mbalimbali zilizo katika wilaya hiyo.
Akiwa ameambatana na
baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo akiwemo mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya
hiyo, watendaji na baadhi ya Madiwani wanaohudhuria kikao kazi
jijini Dar es salaam, Bw. Mapunda
amesema kuwa halmashauri hiyo imejipanga kupunguza utegemezi wa fedha toka
serikali kuu kwa kupanua wigo wa mapato ya ndani kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Amevitaja vyanzo hivyo
kuwa vyanzo hivyo vipya ni pamoja na ushuru wa zao la Ufuta ambalo sasa mapato
yake yamefikia milioni 595, mauzo ya viwanja na ushuru wa Gesi asilia
inayozalishwa katika kijiji cha Songosongo ambayo sasa inatoa asilimia 0.3 ikiwa
ni ushuru wa tozo la huduma.
Akifafanua kuhusu
mapato hayo Bw. Mapunda amesema kuwa katika zao la ufuta asilimia 20 ya pato
hilo inarudishwa vijijini na halmashauri hiyo na kuongeza kuwa mapato ya ushuru
wa huduma unaolipwa kwa halmashauri kutokana na shughuli za gesi za kampuni ya
PAN AFRICAN ENERGY katika eneo la Songosongo huchangia 20% kwa ajili ya
maendeleo ya eneo hilo.
“
Kuanzia mwezi Septemba 2012 Baraza la Madiwani lilipendekeza tuanze kupeleka
asilimia 20 kwenye kijiji cha Songosongo kutokana na malipo ya kampuni ya PAN
AFRICAN ENERGY kiasi cha shilingi milioni 811ambapo hadi sasa tumeshapeleka
jumla ya shilingi milioni 139 na tunajiandaa kupeleka kiasi kingine kilichobaki
cha shilingi 22” ameeleza Bw. Mapunda.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu uboreshaji wa huduma za jamii mkurugenzi huyo amesema kuwa
wilaya ya kilwa inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya Maji Safi,
Umeme, Elimu, mkakati wa kukuza ajira, kuimarisha ulinzi na usalama kwa kujenga
kituo cha polisi cha kisasa kitakachogharimu shilingi milioni 625 na uboreshaji
wa huduma za afya.
Ameongeza
kuwa katika kuboresha huduma za afya wilaya hiyo imeshatenga eneo la hekari 30 kwa
ajili ujenzi wa hospitali ya kisasa yenye hadhi ya kimataifa itakayotoa huduma
ya afya kwa wakazi wa wilaya hiyo.
“Mradi
huu wa hospitali ya kisasa utaanza haraka iwezekanavyo ndani ya mwaka huu hii
ikiwa ni mchango wa rasilimali za eneo letu pia kwa kushirikiana na kampuni
inayochimba gesi, pia tunajiandaa kwa ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa kimataifa
utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.8”
Aidha
katika hatua nyingine Bw. Mapunda ameeleza kuwa halmashauri ya Kilwa inaendelea
na mikakati ya kuimarisha miundombinu ya barabara ili kuimarisha usafiri wa
ndani wa wilaya hiyo, kufanya juhudi ya ukamilishaji wa miundombinu ya ulinzi
na usalama ili kuimarisha hali ya ulinzi na usalama wa miundombinu iliyopo.
No comments:
Post a Comment