NA BASHIR NKOROMO, KALENGA
MWENYEKITI wa Kitongoji cha
Lupembelwasenga, Jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, kwa tiketi ya
Chadema, Ezekiel Kibiki, ameitabiria CCM kumiminiwa kura za kishindo na
wananchi wa kitongoji hicho katika uchaguzi mdogo wa
ubunge utakaofanyika jimboni humo Machi 16, mwaka huu.
Amesema,
uhakika huo anao kutokana na yeye na wananchi wengi wa kitongoji hicho
kubaini kwamba CCM ikiahidi jambo inatekeleza na ndiyo yenye ilani
inayotekelezwa kwa sasa tangu ilipopewa ridhaa na wananchi ya kuongoza
nchi katika uchaguzi mkuu uliopita, tofauti na Chadema ambao alidai
ahadi zao ni za uongo na hawana kazi ya kufanya katika shughuli za
maendeleo.
Mwenyekiti huyo wa kitongoji kwa tiketi ya Chadema, alisema, hayo
leo, Machi 4, 2014, kabla ya kutangaza kuihama Chadema na kujiunga na
CCM, katika mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM uliofanyika kwenye
kitongoji hicho, kumnadi mgombea wa CCM, Godfrey Mgimwa.
"Hivi sasa natangaza kuhama Chadema, na nina kuhakikishieni kwamba
wapo watu wengi nyuma yangu ambao tumeachana na chama hicho na sote kwa
jumla tumeahidi wananchi wa kitongoji chetu kuifanya CCM iibuke na
ushindi wa kishindo kwa kuimwagia kura zetu nyingi katika uchaguzi huu,
anayefikiri natania asubiri ataona baada ya uchaguzi", alisema Kibiki.
Kibiki alisema, yeye na wenzake wameamua kuachana na Chadema baada
ya kubaini kwamba, maneno ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi wa
chama hicho ni ulaghai mtupu ambao ukifuatwa unawapotezea muda wananchi
katika kujiletea maendeleo.
Alisema, baada ya kutafakari kila mmoja kwa wakati wake, wamebaini
kwamba, CCM ndicho chama chenye uhakika wa kusimamia maendeleo yao, kwa
sababu kiliwaahidi kujengwa barabara nzuri na sasa ipo, mbali na mambo
mengine ambayo yametekelezwa kupitia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo la
Kalenga na Waziri wa Fedha Dk. William Mgimwa ambaye alifariki dunia
Januari Mosi, mwaka huu.
Baada ya kutangaza kuachana na Chadema na kujiunga na CCM, Kibiki
alikabidhi kadi yake, kwa Mwenyekiti wa CCM Iringa Vijijini Delfina
Mtavilalo, hatua iliyofuatiwa na wanachama wengine tisa wa Chadema
kutoka kitongoji hicho nao kukabidhi kadi zao kwa Mwenyekiti huyo.
Akizungumza na wananchi kwenye mkutano huo, Mgombea wa CCM katika
uchaguzi huo wa Kalenga, Godfrey Mgimwa alisema, anatambua changamoto
zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, ndiyo sababu amejitolea
kuipeperusha bendera ya CCM ili akipata fursa ya kuchaguliwa asimamie
kuzitatua.
Mgimwa alisema, miongoni mwa changamoto ni uendelezaji wa ujenzi wa
zahanati na shule katika Kitongoji hicho, ambao ulikuwa umeanzishwa na
Mbunge wa zamani Dk. Mgimwa.
Alisema, ana uhakika kwa kupata
ushirikiano wa wananchi na mwongozo wa ilani ya CCM ya mwaka 2010, ana
uhakika changamoto hizo na nyingine zilizopo atapambana nazo hadi
kuhakikisha zinapungua au kwisha kabisa.
No comments:
Post a Comment