Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Itifaki wa
Bunge Maalum la Katiba, Bw. Jossey Mwakasyuka (kushoto) akisisitiza jambo
wakati wa semina iliyoandaliwa kwa ajili ya waandishi wa habari kuhusu
kuimarisha Uandishi wa Habari za shughuli za Bunge iliyofanyika tarehe 6
Septemba, 2014 katika Ukumbi wa African Dreams mjini Dodoma. Kulia ni Mshauri
wa mambo ya Kiufundi toka Shirika la Kimataifa la UNDP, Bi. Anna Kochannesyan.
Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
Kanuni za Bunge Maalum hususani Kanuni ya 77 inawataka
waandishi wa habari kuandika habari za Bunge Maalum kwa weledi mkubwa na
kuzingatia maadili ya uandishi wa habari ili kujiepusha na uandishi wenye
utashi na ushabiki wa kisiasa, msukumo binafsi, chuki ama uchochezi na wakati
mwingine uongo wa makusudi.
Aidha, katika Kanuni hiyo hiyo ya 77(3) inatamka
bayana ya kuwa “Katibu anaweza wakati
wowote kuondoa ruhusa aliyotoa kwa mwakilishi wa Chombo chochote cha habari
iwapo chombo hicho kitatoa taarifa yoyote kuhusu shughuli za Bunge Maalum
ambayo kwa maoni ya Bunge Maalum inapotosha ukweli au vinginevyo inakiuka
Kanuni, taratibu au haki za Bunge Maalum”.
Vyombo vya habari vina haki ya kupata habari ili
viweze kuhabarisha umma juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea nchini has katika
Bunge Maalum la Katiba, lakini katika kufanya hivyo waandishi wa habari wanapaswa
kutenganisha kati ya siasa na uandishi wa habari, hivyo wanapaswa kubainisha na
kuainisha dhana ya uandishi wa habari za kibunge wenye tija kwa taifa ambayo ni
weledi katika uandishi wa habari, uelewa kuhusu matarajio ya wananchi pamoja na
uelewa juu ya dhima na dhamira ya Bunge katika taifa.
Uandishi wa habari ni vema usitumiwe kama njia ya
kufikia malengo ya kisiasa ama mtu binafsi, makundi au chama na kitendo cha
mwanasiasa kuvaa koti la uandishi wakati ni mwanasiasa kunajenga chuki,
kunaharibu heshima ya uandishi wa habari na maisha ya waandishi.
Endapo siasa zitaingizwa katika uandishi wa habari
basi kuna hatari ya kuilisha jamii yetu uongo. Mfano, kifungu cha 25 cha Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba kinavyotafsiriwa kisiasa.
Bila shaka vyombo vya habari ni kama mshipa wa damu wa
siasa na demokrasia nchini. Hakuna chama cha siasa kinachoweza kufanya siasa
kwa ufanisi pasipo kushirikiana na vyombo vya habari, hivyo waandishi wa habari
wanakuwa vijumbe wa kubeba ujumbe wa wanasiasa, kuupeleka kwa wananchi na
kubeba mrejesho wa wananchi na kuupeleka kwa wanasiasa juu ya sera na mienendo
yao.
Akizungumza wakati wa Semina iliyoandaliwa kwa ajili
ya waandishi wa habari kuhusu namna bora ya uandishi wa habari za shughuli za
Bunge, semina iliyoandaliwa na Ofisi ya Habari ya Bunge kwa kushirikiana na
Shirika la Kimataifa la UNDP ambayo ilifanyika tarehe 6 Septemba, 2014 mjini
Dodoma, Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Itifaki wa Bunge Maalum, Bw.
Jossey Mwakasyuka alisema kuwa lengo la semina hiyo ilikuwa ni kuweza kujadiliana na kubadilishana uzoefu juu ya
uandishi wa habari kwa waandishi ili kuweza kuandika habari zilizo sahihi zinazohusu
Bunge hilo kwa manufaa ya taifa.
Katika semina hiyo waandishi wengi watakuwa
wameelimika vya kutosha kwani ni mambo mengi yenye umuhimu yaliwasilishwa na
watoa mada waliobobea katika mambo ya uandishi na siasa hali ambayo itawafanya
waandishi wengi nchini kuzingatia weledi na maadili pindi wanapokuwa wanaandika
habari zinazohusiana na bunge hilo ili kuhabarisha umma.
Katika semina hiyo, watoa mada waliweza kugusia mambo
mbalimbali yakiwemo uandishi wa habari za Bunge na Siasa wenye tija, athari za
siasa katika uandishi wa habari za Bunge, madhara ya Vyombo vya habari
kutumika, miiko na maadili ya kuzingatia katika uandishi huo.
Akitoa mada wakati wa semina hiyo, Mhariri Mtendaji wa
Jamhuri Media Limited, Bw. Deodatus Balile amezitaja athari mbalimbali za siasa
katika uandishi wa habari za Bunge huku akisema kuwa vyombo vya habari vimekuwa
vikitumiwa katika kuzalisha chuki katika jamii kwa kuchochea mbunge Fulani,
Rais, Diwani au Chama Fulani kiangushwe, pia hutumika kuchochea umwagaji damu
na kuondosha amani nchini na lengo kubwa ni kwamba wanasiasa wengi wanafahamu
kuwa vyombo vya habari vinaweza kuwasaidia kuharibu majina ya watu.
Balile aliongeza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kufuata
miiko na maadili ya uandishi wa habari kwa kutofautisha kati ya habari na
maoni, kutoa haki ya asili kwa kila anayetuhumiwa, kuthibitisha habari kupitia
vyanzo vitatu ili habari iwe nzuri lakini pia suala la upendeleo si sehemu ya
habari.
“Usichanganye
wasomaji, wasikilizaji au watazamaji wako kwa maslahi ya kisiasa kwa kutoa
taarifa potofu au picha zisizoakisi ukweli, tujiepushe na athari hizo kwa
kutovaa sare za vyama vya siasa wakati wa kampeni za uchaguzi na tujiepushe na
chuki kwa viongozi ili kuepusha migogoro dhidi yao”, alisema Balile.
Aidha, Balile aliwataka waandishi wajenge urafiki wa
kikazi na wanasiasa lakini si utarishi, ukuwadi wala uwakala bali wawe na
mshikamano, kuhabarisha kuhusu habari za maendeleo, umoja na amani, pia zipewe
kipaumbele na kuepuka kuchapisha habari za uchochezi, lakini mbali na hayo aliwasisitiza
waandishi kuhusu kujiendeleza kielimu na kuzifahamu vyema taratibu, mienendo ya
ripoti za Bunge na matarajio halali ya Wabunge.
Kwa upande wa mtoaji mada mwingine katika semina hiyo,
ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Kamati za Bunge, Bw. Athuman Hussein
aligusia masuala muhimu kwa waandishi hasa kuhusiana na uandishi wa habari za
kibunge wenye tija kwa taifa.
Bw. Hussein alisema kuwa dhana ya uandishi wa habari
wenye tija kwa taifa inajadilika kwa namna nyingi, namna ya kwanza ni
kubainisha tanzu za maudhui na ya pili ni kuainisha nadharia kuhusu maudhui na
kisha kusanisi maarifa. Aidha, alisema pia dhana ya uandishi wa habari za
kibunge wenye tija inahusisha Wabunge na sekretariati, Waandishi wa Habari
pamoja na Msimamizi wa tasnia.
“Hatuwezi
kuwa na uandishi wa habari za kibunge wenye tija kwa taifa kama hatuna weledi
katika uandishi wa habari, hatuelewi matarajio ya wananchi kwa bunge na kama
hatuelewi dhima na dhamira ya Bunge”,
alisema Hussein.
Akizungumiza kuhusu weledi katika uandishi wa habari,
Bw. Hussein alisema kuwa weledi katika uandishi wa habari za kibunge ni jambo
la msingi na hujengwa na kukuzwa kwa tabia ya kujielimisha kuhusu Bunge, tabia
ya kujielimisha kuhusu tasnia ya habari, ufuatiliaji kuhusu matarajio ya
wananchi kwa Bunge pamoja na uelewa kuhusu sayansi ya maadili.
Mtoa mada hapa anamaanisha kuwa hakuna namna ya kuwa
mwandishi wa habari za kibunge mwenye tija kwa taifa kama mwandishi huyo
ameacha kujielimisha kuhusu masuala ya bunge, ameacha kufuatilia ipasavyo
yanayohusu matarajio ya wananchi kuhusu bunge na kama mwandishi huyo hazingatii
mutukutiko katika mazingira ya tasnia aliyopo.
Sambamba na hayo, Bw. Hussein aliendelea kwa kufafanua
juu ya tanzu za weledi katika uandishi wa habari za kibunge akizitaja tanzu
hizo zikiwemo maarifa ya kutosha kuhusu masuala ya kibunge, uelewa mzuri kuhusu
bunge, uelewa kuhusu taratibu, matukio, mila, desturi, mwenendo na misingi,
uelewa kuhusu uwezo wa jamii kupokea na kupokesha, uelewa kuhusu mfumo jamii
uliopo pamoja na uelewa kuhusu hali ya kisiasa na mwenendo wake.
“Msisitizo
ninaouweka katika hili ni kwamba, hakuna anayeweza kuwa mwandishi wa habari za
kibunge kama;- Hana weledi wa uandishi wa habari, lazima aelewe matarajio ya
waandishi, hakuna mwandishi yeyote anayeweza kuleta tija kama haelewi dhima ya
bunge na dhamira ya bunge”, alisisitiza
Hussein.
Uandishi wa habari za kibunge unaweza kuwa mzuri wenye
maadili kama umezingatia madhumuni ya kuripoti habari za kibunge, na yatupasa
kujua kwamba maadili katika uandishi wa habari za kibunge ni kuhusu uamuzi wa
kimantiki unaopendeza kwa mtizamo mpana kuhusu masuala ya bunge.
Jamii nayo inatarajia mambo mengi kutoka katika Bunge
yakiwemo Bunge kutunga sheria zinazokidhi mahitaji ya ustawi wa jamii
zinazotatua pengo la kimfumo wa kisheria kwa maslahi ya umma, bunge linaridhia
mikataba, makubaliano na itifaki zenye tija kwa ustawi wa jamii, pia bunge
linasimamia serikali katika kuhakikisha kuwa inajali mahitaji ya wananchi wake,
inajielekeza kwenye huduma bora za jamii, inajielekeza kwenye misingi ya
utawala na inaepuka ubadhirifu.
Tarajio kubwa lingine ambalo wananchi wanakuwa nalo ni
lile la Bunge kuhidhinisha bajeti ya serikali kwa kuisukuma kwenye mwelekeo wa
kutatua matatizo ya watu, kuimarisha ustawi wa watu pamoja na kuwezesha maisha
bora kwa wananchi.
Uandishi wa habari za kibunge utakuwa na tija iwapo
waandishi wanakuwa na weledi, wanafahamu masuala ya kibunge, wanaelewa
matarajio ya wananchi kiujumla na kitaasisi, hivyo uandishi wa habari za
kibunge ni sehemu ya tasnia ya uandishi wa habari na jambo muhimu katika hilo
ni kujali maadili na weledi kuhusu uandishi na maarifa kuhusu bunge hilo.
Ni vema sasa waandishi tukalisaidia taifa kwa kuandika
habari za kweli kuhusiana na Bunge hili Maalum na kuelimisha umma na
kujiepeusha na ushabiki unaoweza kuliingiza taifa katika matatizo ambayo
kiuhalisia yanayweza kuepukika.
No comments:
Post a Comment