Mwenyekiti wa Forum CC Asasi Mwavuli wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia zinazoshughulika na kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi,Euster Kibona (katikati) akizungumza na waandishi kuhusu kumuomba rais kuchukua hatua dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi Dar es Salaam jana. Mwengine ni Mshauri Mwelekezi Beatrice Kamugisha (kushoto) na Ofisa Mipango Fazal Issa.
Ofisa Mipango wa ForumCC, Fazal Issa (kushoto)
Mwenyekiti wa Forum CC Asasi Mwavuli wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia zinazoshughulika na kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi,Euster Kibona (kushoto) akizungumza na waandishi kuhusu kumuomba rais kuchukua hatua dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi Dar es Salaam.Mwengine ni Ofisa Mipango Fazal Issa.
Dar es
Salaam, Novemba 11, 2015 -
ForumCC ni
asasi mwamvuli wa kitaifa wa asasi za kiraia zinazoshughulika na kupunguza
athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa
kushirikiana na wanachama wake. Kipekee tunachukua
fursa hii kutoa pongezi zetu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania - John Pombe Magufuli; Wabunge na Madiwani wote kwa kuweza
kupata ridhaa ya Watanzania kuongoza serikali ya awamu ya tano.
Tunachukua fursa hii kuwajulisha kuwa tuna matarajio
ya juu kutoka kwao kuwa watatimiza ahadi walizotoa kwa Watanzania. Hii ikiwemo
kushughulikia athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ambazo hazijashughulikiwa
kwa umakini kwa muda mrefu sasa.
Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kubwa
ya maendeleo kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Athari zake zikiwemo kuongezeka kwa joto; ukame; mafuriko;
njaa, ongezeko kubwa la wadudu
waharibifu wa mimea, na magonjwa ya mifugo na binadamu; kukauka kwa vyanzo vya
maji; kuyeyuka kwa theluji ya Mlima Kilimanjaro na mingine; kuzama kwa visiwa muhimu
kwa wavuvi kama Fungu la Nyani na
Maziwe; kuongezeka kwa kina cha bahari; mmonyoko wa fukwe; maji chumvi kuingia
katika nchi kavu. Hivi vyote vina athari kubwa sana katika uchumi, usalama wa
maisha ya Watanzania kwa ujumla.
Hivyo, tunapenda kutoa maombi yetu yafuatayo kwa
Mheshimiwa Rais na uongozi wake:
1. Madhara ya
mabadiliko ya tabianchi ni zaidi ya uharibifu wa mazingira – ni suala la
kiuchumi na kiusalama pia: kwa muda
mrefu sasa suala la mabadiliko ya tabia nchi zimekuwa zikiwekwa kama suala la
kimazingira pekee na hii imekuwa kikwazo kikubwa katika kupambana na changamoto
hii. Suala la mabadiliko ya tabianchi liwekwe kama suala la kiuchumi hususani
kwa nchi yetu ambayo uchumi wake unategemea sana maliasili (kama ardhi, mvua na
misitu). Uchumi wa jamii za kitanzania umekuwa ukiathirika sana katika sekta mbalimbali
ikiwemo kilimo, mifugo, maji, miundombinu na nishati. Hali ambayo inaongeza
umasikini kwa jamii kwa kasi kubwa sana.
2.
Kuweka
jitihada za dhati katika upatikanaji na ukusanyaji wa fedha za maendeleo: ili
kuhakikisha mipango na mikakati ya kimaendeleo ya kupambana na athari za mabadiliko
ya tabianchi na kuboresha uchumi; jitihada za dhati zinahitajika kufanyika kwa Serikali katika upatikanaji na ukusanyaji wa
fedha za miradi ya maendeleo kwa ngazi zote. Hii ikiwemo kuziba mianya ya rushwa
na ubadhilifu; na pia kuongeza uwezo wa wahusika katika kubuni njia mbalimbali
za upatikanaji wa pato la Serikali kitaifa na ngazi ya Serikali za Mitaa.
Kuweka
mfumo madhubuti wa kufuatilia upatikanaji na matumizi ya fedha za kupambana na
athari za mabadiliko ya tabianchi zinazopatikana
kwa vyanzo vya ndani na jumuiya ya kimataifa ambavyo ni vingi zaidi. Kwa sasa nchi yetu haina mfumo mahususi wa ufuatiliaji wa
vyanzo hivyo hususani katika bajeti ya taifa. Hivyo, tunasisitiza
kuwe na mfumo mahususi na madhubuti wa
ufuatiliaji ikiwemo kuweka “Code” maalum ya mabadiliko ya tabianchi katika
bajeti. Hii itasaidia kuboresha uwazi, uwajibikaji na pia kuvutia wahisani na
uwekezaji katika eneo hilo.
Kuhakikisha bajeti ya kilimo
inakuwa zaidi ya 10% ya bajeti yote kwa mwaka kama inavyoagizwa na
mkataba wa Maputo na Malabo 2014 ambapo Tanzania iliridhia. Bajeti hiyo itolewe
kwa wakati na ifike kwa walengwa ambao ni wakulima wadogo wadogo ili
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo upatikanaji wa mbegu
bora, wataalam, miundombinu ya umwagiliaji wa teknolojia ya matone.
3.
Usimamizi
wa kikamilifu na uratibu katika utekelezaji wa mipango, mikakati na miradi ya
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi: Tunatoa
rai kwa Mheshimiwa Waziri husika kushughulikia kikamilifu swala la mabadiliko ya
tabianchi ambalo lipo chini ya ofisi yake kwa kuimarisha uratibu na utendaji wa
taasisi zote zenye jukumu la kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi;
4.
Kuimarisha
miundombinu na uhifadhi wa taka ngumu katika miji mikubwa ili
kuhakikisha mafuriko hayaleti madhara katika shughuli za kiuchumi na ustawi wa
jamii;
5.
Kuboresha mfumo wa ushirikishwaji wa kikamilifu wa wadau na wananchi
kiujumla katika mipango na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayohusiana na
mabadiliko ya tabianchi.
Imetolewa na:
ForumCC
S.L.P 105270 - Dar es Salaam
+255 759/658 266 326
No comments:
Post a Comment