Na Mwandishi wetu – Maelezo
Serikali imeshauriwa kuiomba China kutekeleza ahadi yake ya kufunga
masoko yote ya meno ya Tembo ili kuweza
kulinda usalama wa muda mrefu wa wanyama
hao kwani nchi hiyo ni mtumiaji
mkubwa wa meno hayo na kwa kufunga
biashara hiyo kutapelekea kuanguka kwa
haraka kwa biashara katika sehemu nyingine ulimwenguni.
Ombi hilo limetolewa leo na
Taasisi inayopinga uwindaji haramu wa
tembo wakati wakisoma barua yao ya wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano
wa Idara ya Habari uliopo jijini Dar es Salaam.
Akisoma barua hiyo Shubert
Mwarabu ambaye ni mratibu wa kampeni ya okoa Tembo wa Tanzania alianza
kumpongeza Mhe. Rais kwa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano na kuisihi Serikali
kutumia urafiki wa kihistoria kati yake na China kufunga masoko ya meno ya Tembo yaliyopo
nchini China.
Alisema takribani asilimia 90 ya
meno ya Tembo toka Tanzania yanauzwa China, ambapo biashara halali ya meno ya
Tembo inatumika kama mwavuli wa biashara haramu ya meno ya Tembo ambacho ndio chanzo
kikuu cha tatizo la ujangili wa Tembo.
“Tunakuandikia barua leo kukuomba
kuchukua hatua juu ya suala la kupungua kwa kasi idadi ya Tembo nchini kutokana
na ujangili kwa ajili ya biashara haramu ya meno ya Tembo”.
“Kutokana na Ripoti ya Sensa ya TAWIRI
2014 Miaka hamsini iliyopita, kulikuwa na Tembo 300,000 nchini Tanzania. Mwaka
2009, kulikuwa na Tembo 109,000. Leo, inakadiriwa kuna Tembo 43,000 tu
waliobaki – upungufu wa asilimia 60 ndani ya miaka mitano tu”, alisema Mwarabu.
Aliendelea kusema wanatambua hatua
zilizofanyika kukabiliana na tatizo la ujangili. Uundaji wa mikakati ya kitaifa
dhidi ya ujangili, juhudi za Kikosi Kazi cha National and Transnational Serious
Crimes Investigation Unit (NTSCIU) na kuongeza rasilimali kwa mamlaka ya wanyamapori
ni hatua muhimu.
Alisisitiza, “Nchi yetu imekuwa
mstari wa mbele katika uhifadhi wa Tembo hapo kabla. Mwaka 1989, Tanzania
iliongoza jitihada za kupiga marufuku biashara ya meno ya Tembo ulimwenguni tulipochukua
hatua kukomesha mauaji ya Tembo, dunia nzima ilituunga mkono. Ni lazima
turejeshe upya dhamira yetu kwa ahadi tuliyojiwekea kwa hatua ya kimataifa
zaidi ya miaka ishirini iliyopita, na kuleta ukomo wa biashara yote ya meno ya
Tembo”.
“Tunaiomba
serikali kuwakamata na kuwashitaki wafanyabiashara wakubwa wa meno ya Tembo
nchini, bila kujali utaifa, hadhi au mamlaka, kuteketeza hadharani ghala ya
meno ya Tembo Tanzania – inayosadikika kuwa kubwa kuliko yote ulimwenguni kwani
ni gharama
kutunza na kulinda ghala la meno ya Tembo Tanzania”.
No comments:
Post a Comment