Na Anna Nkinda – Maelezo, Mwanza
Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) zimetakiwa kuwahimiza wanachama wao hasa vijana waliopo ndani ya vikundi vyao kuitumia mikopo wanayoipata katika shughuli za
kilimo cha chakula, ufugaji wa samaki na uvuvi ili kuisaidia nchi
kuepukana na tatizo la njaa kwani vijana ni nguvu kazi ya taifa.
Wito huo umetolewa leo jijini Mwanza na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara wakati alipozitembelea SACCOS za Mwanza na Wafanyabiashara Wadogowadogo Mkoa wa Mwanza (WADOKI) ambazo zilizopata pesa za mkopo kutoka mfuko wa Maendeleo ya Vijana kupitia Halmashauri ya jiji.
Dk.
Mukangara alisema kuwa Wizara yake kupitia Halmshauri za wilaya
itahakikisha kuwa mashamba yanapatikana ili vijana waweze kujihusisha na
kazi za kilimo jambo litakaloifanya nchi kuwa na uhakika wa kupata
chakula cha kutosha kwani ni aibu kwa taifa kukumbwa na njaa wakati kuna vijana wengi wanazunguka mitaani kwa kigezo kuwa hawana kazi za kufanya.
“Ardhi ipo ya kutosha ni
kiasi cha SACCOS kuamua kuwa hivi sasa vijana watakaochukua mkopo
watatumia fedha hizo katika kazi za kilimo, uvuvi na ufugaji wa samaki
tunafahamu kuwa shughuli hizi zinahitaji pembejeo Wizara yangu kupitia Idara ya vijana itashirikiana na kusaidiana nanyi kwa kuwa SACCOS zenu zinawalenga vijana hivyo basi tumieni fursa zinazowazuguka”, alisema Dk. Mukangara.
Kwa
upande wa ulipaji madeni ya mikopo kwa wanachama, Dk. Mukangara
alizitaka SACCOS hizo kuwajengea wanachama wao hasa vijana tabia ya
kulipa mikopo kwa wakati na kuwahimiza kulipa kodi wanazotakiwa kulipa kwa kufanya hivyo wawatambua kuwa huduma wanazozipata kutoka Serikalini zinatokana na kodi yao wenyewe.
Akisoma taarifa ya WADOKI SACCOS Deograthias Peter ambaye ni Meneja alisema kuwa hivi
sasa wanawanachama vijana 550 kati ya hao wanawake ni 335 na wanaume
215 wanaojishughulisha na kazi mbalimbali za uzalishaji mali katika
harakati za kuondokana na umaskini.
“Mkopo wa vijana ulikuwa ni mzuri hasa kwa wale ambao kipato chao ni cha chini. Kupitia mkopo huu tuligundua kuwa kuna
uhitaji mkubwa wa fedha hasa kwa vijana ambao hawana ajira na kama
wakiwezeshwa wanaweza wakafanya vizuri na kuinua hali zao za maisha.
Kwakuliona hilo tulianzisha mpango wa kutafuta vikundi vya
vijana na hadi sasa wanachama vijana wameweza kujipatia ajira kwa
kutumia mikopo wanayoipata kutoka WADOKI na kuinua hali zao za maisha”,
alisema Peter.
Kwa upande wake Meneja wa Mwanza SACCOS James Nyakiha alisema kuwa fedha za mkopo wa vijana zilizotolewa ni ndogo kwani
vijana ni wengi hivyo fedha hizo hutolewa kwa wanachama wachache hali
inayoleta hisia ya baadhi ya wanachama kuwa mkopo umetolewa kwa ubaguzi
na muda wa mkopo wa mwaka mmoja mmoja kwa SACCOS hautoi fursa kwa ya kuwahudumia wanachama wengi vijana.
SACCOS
hizo zilipokea mkopo wa vijana mwaka 2009 kiasi cha shilingi milioni
tano kwa kila kikundi toka Idara ya Vijana kupitia Halmashauri ya jiji
ambao ulitolewa kwa wanachama vijana 12 kutoka SACCOS ya WADOKI na
vijana 21 kutoka SACCOS ya Mwanza ambao wamesharejesha mkopo huo.
Waziri huyo alizitembelea SACCOS hizo ambazo ni baadhi ya SACCOS za mkoa huo zilizopata mkopo wa vijana ili kuona fedha hizo zimewezaje kuwasaidia vijana
kama kundi na kijana mmojammoja waliopata mkopo huo. Katika Mkoa wa
Mwanza jumla ya vikundi 14 vilipata mkopo wa vijana ambapo kila SACCOS
ilipata shilingi milioni tano na kuzifanya fedha zilizotolewa katika mkoa huo kufikia shilingi milioni 70.
No comments:
Post a Comment