Waraka
wa marekebisho ya Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
umepita baada ya kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa Mkutano
Mkuu waliopiga kura.
Jumla
ya wajumbe waliopiga kura kwa njia hiyo ya waraka ni 103 ambapo 70
wameunga mkono wakati waliokataa ni 33. Idadi hiyo ni asilimia 68 ya
kura zote zilizopigwa, hivyo kupatikana theluthi mbili ya kura
zilizopigwa ili kufanya marekebisho kikatiba.
Kura
zilizosema ndiyo kutoka kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa vyama vya mikoa
ni 46, wajumbe kutoka vyama shiriki ni 13 wakati klabu za Ligi Kuu
zilizounga mkono ni kumi na moja.
Kamati
ya Utendaji ya TFF inawashukuru wajumbe wote wa Mkutano Mkuu- kwa
waliounga mkono na waliokataa kwa vile walikuwa wanatekeleza wajibu wao
wa kikatiba.
Vipengele
vilivyoingizwa ni ‘club licencing’ kama ilivyoagizwa na Shirikisho la
Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF kama
ilivyoshauriwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na
kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Vilevile
Kamati ya Utendaji itakutana Desemba 23 mwaka huu kufanya marekebisho
ya Kanuni za Uchaguzi, kutokana na kupitishwa kwa marekebisho hayo
ambayo yanaunda Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF. Pia itachagua
wajumbe wa Kamati ya Rufani ya TFF.
Mkutano
Mkuu wa TFF ambapo pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi utafanyika
Februari 23 na 24 mwakani. Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, wajumbe
wanatakiwa kupewa taarifa ya Mkutano Mkuu siku 60 kabla.
MIKOA SITA KUTOSHIRIKI UCHAGUZI TWFA
Mikoa
sita ambayo ni wanachama wa Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake Tanzania
(TWFA) haitashiriki katika uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika Desemba
19 mwaka huu mjini Morogoro.
Kwa
mujibu wa taarifa ya TWFA, wanachama hao hawatashiriki kwa vile hadi
sasa haijapokea taarifa za uchaguzi kwenye vyama hivyo. Vyama hivyo ni
vya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Rukwa, Shinyanga na Tabora.
Uchaguzi
huo utafanyika kwenye hoteli ya Midland, na wagombea ni Isabela Kapera,
Joan Minja na Lina Kessy (Mwenyekiti), Rose Kissiwa (Makamu
Mwenyekiti), Amina Karuma na Cecilia Mkafum (Katibu Mkuu), Zena Chande
(Mjumbe Mkutano Mkuu wa TFF) na Sophia Charles na Triphonia Temba
wanaowania ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment