Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imeahidi wadau wa mchezo huo kuwa itafanya kazi zake kwa misingi ya
haki.
Akizungumza
baada ya uzinduzi wa Kamati hiyo uliofanywa Dar es Salaam leo mchana
(Januari 23 mwaka huu) na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kwa niaba
ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga, Mwenyekiti wa Kamati hiyo yenye wajumbe
watano Idd Mtiginjola amesema wapo kwa ajili ya kutenda haki.
Mtiginjola
amesema Kamati yao inaundwa na watu waadilifu, hivyo watafanya kazi kwa
kuzingatia kanuni zilizopo na sheria nyingine za mpira wa miguu ikiwemo
Katiba husika.
“Niwakikishie
kuwa hatutafanya uamuzi kutokana na mawazo yetu, tufanya uamuzi kwa
kuzingatia kanuni na sheria. Kamati hii ni chombo cha haki, hivyo
itafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria. Sheria na haki ni vitu viwili
tofauti. Sheria zipo kwa ajili ya kuitafuta haki,” amesema Mtiginjola
ambaye kitaaluma ni Mwanasheria akiwa ni Wakili wa Kujitegemea.
Baada
ya uzinduzi, Osiah aliwakabidhi wajumbe wa kamati hiyo vitendea kazi
(instruments) mbalimbali zikiwemo kanuni za uchaguzi za TFF na wanachama
wake, Katiba ya TFF na Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA).
Mbali
ya Mtiginjola, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Makamu
Mwenyekiti, Francis Kabwe ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Rufani ya
Tanzania, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mohamed Mpinga ambaye pia
kitaaluma ni Mwanasheria.
Mshambuliaji
wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo ambaye kwa
sasa ni Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)
kilichopo mjini Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu ambaye pia ni
Mbunge wa Kilwa Kaskazini.
MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kesho (Januari 24 mwaka huu) saa 6
kamili mchana litakuwa na mkutano na waandishi wa habari.
Mkutano huo utafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment