Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh akipokea cheti cha kukamilika kwa mradi wa kuiunganisha ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka kwa Bw. Kisamba Tambwe (kulia) Meneja wa njia za Mawasiliano za nje kutoka Kampuni ya simu Tanzania.
Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh (katikati mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Ofisi hiyo na viongozi wa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL leo jijini Dar Es salaam.
OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI WA HESABU ZA SERIKALI YAUNGANISHWA KWENYE MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO.
Na. Aron Msigwa -MAELEZO.
Ofisi yaTaifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali
imeingia katika mfumo mpya wa mawasiliano wa matumizi ya barua pepe na
intraneti utakaoiwezesha ofisi hiyo kutuma na kupokea taarifa za
utendaji kwa haraka kufuatia kukamilika kwa mradi wa kuunganishwa kwenye
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam wakati wa makabidhiano ya mradi huo uliofanywa na kampuni ya
Simu Tanzania, Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw.
Ludovick Utouh amesema kuwa mradi huo utaiwezesha ofisi yake kuimarisha
mawasiliano ya ndani na nje ya ofisi kupitia mfumo wa intaneti.
Amesema mradi huo ambao kwa sasa umeanza kwa
kuziunganisha ofisi 12 za mikoa mbalimbali utaleta mabadiliko makubwa
katika nyanja nzima ya upashanaji habari na utawawezesha watumishi wa
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za serikali kupata mawasiliano kwa
kwa haraka na usalama zaidi kupitia makao makuu ya ofisi hiyo.
Amesema mkongo wa taifa utaiwezesha ofisi hiyo
kumiliki na kudhibiti taarifa mbalimbali zinazotumwa kwa kuwatumia
wataalam wa Tehama wa ndani huku akibainisha kuwa mfumo huo mpya
utawazuia watumishi wa ofisi hiyo kutumia mifumo ya kawaida ya barua
pepe na mitandao hatarishi inayoweza kuleta madhara kwenye taarifa
muhimu za serkali.
" Mradi huu umekamilika wakati muafaka kwa sababu
utatuwezesha kupunguza gharama, kumiliki na kudhibiti sisi wenyewe
taarifa zetu za kiutendaji za kila siku kupitia wataalam wa Tehama
tulionao katika ofisi zetu na kuondoa kabisa mfumo uliokuwepo wa kubeba
taarifa mikononi kutoka eneo moja hadi jingine" amesema Utouh.
Amefafanua kuwa kukamilika kwa mradi huo
kutaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali nchini
kujenga uwezo wa uimarishaji wa miundombinu za shughuli za Ukaguzi na
utendaji na kurahisisha mawasiliano kwa kutumia mfumo wa kompyuta huku
akifafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Tanzania
kwa kipindi cha miaka 6 ni wakaguzi wa Umoja wa mataifa ukaguzi
unaofanywa katika miji mbalimbali duniani.
Utouh amebainisha kuwa ofisi yake sasa itaweza
kufanya mikutano ya kiutawala moja kwa moja na ofisi za mikoani kupitia
mfumo mpya wa mawasiliano wa mtandao (video conference) na kuwataka
watumishi wa ofisi hiyo kuutumia ipasavyo mfumo huo kwa manufaa ya
taifa.
Kwa upande wake Meneja wa njia za mawasiliano ya nje
wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Bw. Kisamba Tambwe akikabidhi mradi
huo amesema kuwa kampuni hiyo imetekeleza mradi huo kwa ufanisi mkubwa
ili uweze kukidhi malengo yaliyokusudiwa.
Amesema TTCL itaendelea kuhakikisha kuwa ofisi 12
za mikoa iliyouganishwa kwenye Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa zinakuwa
na usambazaji salama wa taarifa kutoka eneo moja hadi jingine.
No comments:
Post a Comment