Wachezaji
wawili kutoka Tanzania wamechaguliwa miongoni mwa 50 waliofanyiwa
majaribio nchini Uganda kwa ajili ya kuingia katika kituo cha kuendeleza
vipaji (centre of excellence) kilichoko Doha nchini Qatar kupitia
mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream.
Abdulrasul
Tahir Bitebo (15) ambaye ni mshambuliaji kutoka Kituo cha Uwanja wa
Karume, na Martin Omela Tangazi (14) ambaye ni beki kutoka Kituo cha
Ukonga ndiyo waliochaguliwa kutoka Tanzania kuingia katika kituo ambapo
watakaa kwa mwezi mmoja kabla ya kusaini mkataba rasmi wa kuendelezwa.
Wachezaji
wengine walikuwa wakitoka katika nchi za Uganda na Kenya. Mchezaji
mwingine aliyefuzu katika nafasi tatu zilizokuwepo ni kutoka nchini
Kenya.
Mpango
wa Aspire Football Dream unafadhiliwa na Mtoto wa Mfalme wa Qatar
katika nchi 16 duniani, na kwa hapa nchini uko chini ya Idara ya Ufundi
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
TFF
ina jumla ya vituo 14 vya kuendeleza vipaji kupitia mpango huo wa
Aspire Football Dream. Vituo hivyo ni Karume, Kigamboni, Tandika, Kawe,
Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Makongo, na Tabata vilivyo katika
Mkoa wa Dar es Salaam. Vingine ni Bagamoyo kilichopo mkoani Pwani,
Morogoro, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kituo kingine cha kuendeleza vipaji (centre of excellence) cha Aspire kipo Dakar nchini Senegal.
TFF KUENDESHA KOZI SITA KATI YA JULAI- SEPTEMBA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaendesha kozi sita tofauti za mpira wa miguu kati ya Julai na Septemba mwaka huu.
Kozi
hizo ni FIFA 11 For Health itakayofanyika Hombolo mkoani Dodoma kuanzia
Julai 8 hadi 19 mwaka huu. Julai 6 hadi 15 mwaka huu kutakuwa na kozi
ya mpira wa miguu wa ufukweni (Beach Soccer) itakayofanyika jijini Dar
es Salaam.
Waamuzi
wa FIFA nao watakuwa na kozi itakayofanyika kati ya Agosti 22 hadi 26
mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati kozi ya ukocha kwa ajili ya Copa
Coca-Cola itafanyika jijini Dar es Salaam kati ya Agosti 12 na 17 mwaka
huu.
Vilevile kutakuwa na kozi ya mpango
wa grassroots unaolenga wachezaji mpira wa miguu (wasichana na
wavulana) wenye umri kuanzia miaka 6-12 itafanyika kuanzia Septemba 9
hadi 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati tamasha (festival) la
grassroots litafanyika Uwanja wa Karume, Septemba 14 mwaka huu.
RCL KUKAMILISHA HATUA YA NNE JUMAPILI
Mechi
za marudiano za hatua ya nne ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL)
zitachezwa Jumapili (Juni 30 mwaka huu) kwenye viwanja vya Sokoine
jijini Mbeya, na Kambarage mjini Shinyanga.
Friends
Rangers ya Dar es Salaam ambayo katika mechi ya kwanza ilifungwa
nyumbani mabao 3-0 itakuwa mgeni wa Stand United FC mjini Shinyanga
wakati Kimondo SC itaikaribisha Polisi Jamii ya Mara jijini Mbeya.
Katika mechi ya kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
Hatua
ya mwisho ya RCL itachezwa Julai 3 mwaka huu kwa mechi za kwanza wakati
zile za marudiano zitafanyika Julai 7 mwaka huu. Timu tatu za kwanza
zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment