Na.
Benedict Liwenga-MAELEZO
VIJANA nchini
wametakiwa kujiunga na vikundi vya ujasiriamali na Vyama vya kuweka akiba na
kukopa (SACCOS) kama njia ya kujipatia mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli
zao za uzalishaji mali ili waweze kupata mikopo ambayo itawasaidia kujikwamua
kimaisha.
Wito huo umetolewa jana
na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara wakati
akiongea na Vijana wa Kikundi cha Mambo
Safi kilichopo kata ya Kimara jijini Dar
es Salaam.
Waziri Dkt. Mukangara
alisema kuwa katika jitihada za kuwawezesha vijana kuendeleza shughuli zao za
uzalishaji mali Serikali kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana na kwa
kushirikina na vyombo vya fedha na wadau wengine itaendelea kuhakikisha kuwa wanatoa
mikopo yenye masharti nafuu kwa
wajasiriamali wadogo wadogo.
“Tutaendelea pia
kuwahimiza na kuwatayarisha vijana waliomaliza vyuo vikuu na walio nje ya vyuo
kuhakikisha kuwa wanajiunga katika
vikundi mbalimbali vya nguvu kazi ili kujiletea maendeleo.
“Kwani katika umri wa
ujana, mnaweza kufanya mambo makubwa na mazuri kwa kutumia nguvu mliyonayo,
wengi wenu mna uwezo mkubwa wa kufikiri kwa kutumia teknolojia za kisasa na
kuchanganua mambo pia mchangamkie fursa mnazokutana nazo kila siku”, Alisema Dkt Fenella.
Aidha Dkt. Mukangara
amewaasa vijana kutii sheria za nchi na kuheshimu vyombo vya dola kwani hakuna
nchi yoyote hapa duniani ambayo chombo
chake cha dola kikiguswa itanyamaza.
“Lakini kubwa kabisa ni
kujenga na kutunza nidhamu yenu na kutii sheria na vyombo vya Dola ili
tuendelee kudumisha amani na kujiletea maendeleo”. Dkt. Fenella alisema.
Akisoma taarifa ya kikundi hicho
Phabbian Salvatory ambaye ni Mkurugenzi wa kikundi alisema kuwa kazi wanazozifanya ni kutoa darasa la mafunzo ya kila siku ya sanaa za jukwaani,uzalishaji,maadili, mazingira
na afya, kuhamasisha na kutoa burudani kwa njia ya matamasha,kongamano na
semina.
Kazi zingine ni kuwafikia vijana popote
walipo na kubaini kero zilizopo, kutoa mafunzo
ya ujasiriamali,afya,mazingira, maadili kwa rika tofauti na kujitolea kwa
shughuli tofauti za kijamii na Serikalini pale wanapohitajika.
Salvatory alizitaja changamoto
zinazowakabili kuwa ni pamoja na kufanya kazi katika mazingira magumu ya ukosefu wa fedha na vitendea kazi ,
kudharauliwa na jamii inayowazunguka kuwa sanaa ni uhuni, ukosefu wa mtaalamu
wa kuandika miradi, kutokuwa na mwanasheria
wa kusimamia kazi zao kisheria na ugumu
wa vijana katika mapokeo ya shuhguli
tunatozozifanya.
“Pia tunakabiliwa na changamoto ya vijana
kukosa subira na mtazamo potofu, ahadi hewa zinazotolewa na viongozi pasipo
kutekeleza kwa wakati , kutokupewa fursa zilizoko serikalini za kitaifa na kimataifa ambako kunapelekea
vijana wengi kukata tamaa na kuondoka katika taasisi kwani maisha yao
wanategemea hapa na kazi zetu kudhulumiwa na watu mbalimbali.
Waziri Mukangara alitoa
zawadi ya Mashine moja ya kutolea kopi aina ya Kyocera, Kompyuta Mpakato
(Laptop) moja aina ya Samsung, Mipira 22 kwa kikundi hicho pia alitoa zawadi ya Jezi seti mbili na Mipira 2 kwa vijana wa
Mabibo jijini Dar es Salaam, vitu vyote hivyo
vinathamani ya shilingi Milioni
3.7.
Kikundi cha mambo safi kilichosajiliwa kisheria
na baraza la sanaa la taifa (BASATA) mwaka 2008 kwa ajili ya kuendesha
shughuli za vijana na uchumi ,sanaa,michezo na maendeleo ya jamii.
No comments:
Post a Comment