Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kesho,
Jumamosi, Agosti 3, 2013 atakutana na kufanya mazungumzo ya faragha na rasmi na
Rais wa 42 wa Marekani,
Mheshimiwa Bill Clinton ambaye anawasili nchini kwa
ziara kesho mchana. Baada ya mazungumzo hayo, yatakayofanyika Ikulu, Dar Es
Salaam, Rais Kikwete na Mheshimiwa Clinton watashuhudia utiaji saini wa
makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Taasisi ya Clinton Foundation
ambako taasisi hiyo itasaidia juhudi za Tanzania kuendeleza kilimo.
Sherehe za
kutia saini makubaliano hayo pia zitafanyika Ikulu. Rais Clinton yuko katika
ziara ya baadhi ya nchi za Afrika ambazo zinashirikiana na taasisi yake katika
kutafuta majawabu ya changamoto za maendeleo.
Katika Tanzania, Clinton
Foundation imechangia kwa kiasi kikubwa jitihada za maendeleo katika nyanja ya
afya na kilimo ikiwa ni pamoja na kusaidia kupatikana kwa dawa za kurefusha
maisha kwa wanaoishi na virusi.
No comments:
Post a Comment