Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea zawadi inayotokana na zao la mnazi toka kwa Waziri wa Maendeleo ya Minazi na Maendeleo ya Shamba la Janatha wa Sri Lanka, Mheshimiwa Jagath Pushpakumara (shati jeupe) na ujumbe wake mjini Colombo, Sri Lanka, kuzungumzia njia za kushirikiana kukabiliana na maradhi ya mazao likiwamo zao la mnazi ambalo linakabiliwa na tatizo la mnyauko.
Picha ya pamoja ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati na Waziri wa Maendeleo ya Minazi na Maendeleo ya Shamba la Janatha wa Sri Lanka, Mheshimiwa Jagath Pushpakumara (shati jeupe) na ujumbe wake mjini Colombo, Sri Lanka, kuzungumzia njia za kushirikiana
kukabiliana na maradhi ya mazao likiwamo zao la mnazi ambalo linakabiliwa na tatizo la mnyauko.
PICHA NA IKULU
Rais
Kikwete akabidhiwa ripoti kuhusu ugonjwa wa mnyauko wa minazi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali imedhamiria kukabiliana na maradhi ya mazao
likiwamo zao la mnazi ambalo linakabiliwa na tatizo la mnyauko.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni muhimu kwa
Serikali kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo la minazi kwa sababu watu wengi
katika baadhi ya maeneo ambayo uchumi wake unategemea zao la mnazi wanakabiliwa
na hatari ya kweli kweli ya kuathirika kwa maisha yao.
Rais Kikwete ametoa uhakikisho huo jana,
Jumamosi, Novemba 16, 2013, wakati alipokutana na Waziri wa Maendeleo ya Minazi
na Maendeleo ya Shamba la Janatha wa Sri Lanka,
Mheshimiwa Jagath Pushpakumara na ujumbe wake mjini Colombo. Waziri huyo aliandamana na
Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti ya Minazi ya Sri Lanka.
Rais Kikwete yuko nchini Sri Lanka kuhudhuria Mkutano wa
Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Madola (CHOGM) unaomalizika leo, Jumapili,
Novemba 17, 2013. Mkutano huo wa siku tatu, ulianza juzi, Ijumaa, Novemba 15,
2013.
Mheshimiwa Pushpakumara na ujumbe wake
walikuwa wanamwelezea na kumkabidhi Rais Kikwete Ripoti ya Magonjwa ya Minazi
iliyoandaliwa na wataalam wa minazi wa Sri Lanka ambao walitembelea
Tanzania Julai mwaka huu.
Wataalam hao walitembea Tanzania na kufanya utafiti kuhusu
ugonjwa unaolikabili zao la minazi kufuatia ahadi ya Rais Mahinda Rajapaksa
aliyoitoa kwa Rais Kikwete wakati alipofanya ziara rasmi ya Tanzania Juni 27,
2013, na baadaye kushiriki katika Mkutano wa Smart Partnership Juni mwaka huu.
Rais Rajapaksa alitoa ahadi hiyo baada ya
kuelezwa na Rais Kikwete kuhusu zao la kukauka kwa minazi nchini. Mnazi ni zao
muhimu sana katika uchumi wa Sri Lanka na ni zao tegemeo kwa wananchi wa
Taifa-Kisiwa hilo kilichoko kusini mashariki mwa
India
katika Barahri ya Hindi.
Wataalamu waliofuatana na Waziri huyo
wamemwambia Rais Kikwete kuwa ugonjwa unaolikabili zao hilo
la minazi ambao pia unashambulia minazi katika eneo la Caribbean
hauna tiba kwa sababu mpaka sasa hakuna taasisi yoyote ya utafiti imegundua
dawa hiyo.
Wataalam hao ambao walikaa Tanzania kwa wiki
moja, zikiwamo siku mbili katika Zanzibar, wanasema kuwa zao hilo la mnazi,
kama ilivyo katika nchi nyingine zinazolima zao hilo, lina uwezo mkubwa wa
kusaidia uchumi kupitia viwanda vidogo vidogo.
Wakati wakiwa Tanzania,
wataalam hao wa Sri Lanka
walifanya uchunguzi na utafiti kwa karibu na wataalam wa Taasisi ya Utafiti ya
Kilimo ya Mikocheni (MARI).
No comments:
Post a Comment