Na Anna Nkinda- Cape Town , Afrika ya Kusini
Jamii imetakiwa kushirikiana
kwa pamoja na kuchukua hatua za karibu
kwa kuwalea watoto wa kike kama watoto wao wa kuwazaa huku wakiwapa nafasi kama watoto wa
kiume, kuwapatia elimu, kuwaheshimu na kuwalinda jambo ambalo litawafanya wafanikiwe
katika maisha yao.
Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati
akiongea kwenye mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na
elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki
(EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa
Afrika (SADC) unaofanyika katika Hoteli ya The Westin iliyopo mjini Cape
Town nchini Afrika ya Kusini.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema tafiti zinaonyesha Duniani kote zaidi ya wasichana
milioni 58 wameolewa wakiwa na umri wa chini
ya miaka 18 kati ya hao milioni 15 wanaumri wa kati ya miaka 10 hadi 14 huku
wengi wao wakiwa wameolewa kinyume na matakwa yao na kushuhudia unyanyasaji
wa kijinsia, uelewa mdogo wa haki zao na kutopata elimu ya
afya ya uzazi.
“Idadi ya watoto wa kike wanaomaliza
elimu ya msingi imeongezeka na kuwazidi watoto wa kiume ingawa idadi ya
wasichana wanaomaliza elimu ya Sekondari ni ndogo ukilinganisha na watoto wa
kiume katika nchi nyingi za Afrika”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa maambukizi mapya ya Virusi
vya Ukimwi Mama Kikwete alisema asilimia
42 ya watu wanaopata maambukizi ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi
24, katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara vijana ni asilimia 80.
Mama Kikwete alisema, “Nchini Tanzania tafiti
zilizofanyika zimeonyesha kuwa watoto wa kike wengi wanajihusisha na mahusiano ya kimapenzi mapema kwa asilimi
13 ambao wanafanya mapenzi kabla ya umri
wa miaka 15 na kwa upande wa watoto wa kiume ni asilimia saba matokeo yake ni
upatikanaji wa mimba za utotoni.
Msichana mmoja kati ya wasichana wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ni
mjamzito au ameshazaa. Idadi hii ni
kubwa katika nchi nyingi za Afrika inasikitisha kwani kubeba mimba katika umri mdogo kunaweza
kusababisha kifo cha mama mjamzito pamoja
na mtoto wakati wa kujifungua”.
Akifungua mkutano huo wa siku mbili Mkurugenzi
wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa
la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) Prof.
Sheila Tlou alisema wajumbe wa kamati hiyo wanatakiwa kuhakikisha maazimio waliyokubaliana
yanapitishwa na kufanyiwa kazi katika
nchi husika ili vijana waweze kupata elimu ya afya ya uzazi.
Prof. Tlou alisema, “Tutahakikisha kuwa
rasilimali za kutosha zinapatikana ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha kutoka kwa
wafadhili mbalimbali hii ni kuhakikisha kuwa
maadhimio haya yanafanikiwa kwani vijana ni viongozi wa leo wanaohitaji kupata huduma
ikiwa ni pamoja na elimu ili waweze kujiepusha na mazingira ambayo yatawapelekea
kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi”.
Kwa upande wake Naibu
Katibu Mkuu wa EAC Jesca Eriyo alisema mwaka mmoja uliopita wakuu wa nchi za
Afrika ya Mashariki walikubaliana kuhakikisha wanaimarisha utolewaji wa elimu ya afya ya uzazi katika
nchi zao na hivyo kuwa rahisi kwa nchi hizo kufanyika kazi maazimio hayo.
“Vijana wanamaswali
mengi kuhusu afya ya uzazi na inafika wakati hawajui wa kumuuliza hivyo basi elimu ya uzazi
ifundishwe kwao kwani kutokana na mila za kiafrika ni vigumu kwa mzazi kuongea na mtoto wake kuhusu
afya ya uzazi”, alisema Eriyo.
Alimalizia kwa kusema
kuwa vijana wanatakiwa kujua hali ya afya zao ikiwa ni pamoja na kupima kama
wamepata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
na kujiepusha na wababa na wamama (mafataki) ambao wanaweza kuwarubuni na
kuwaharibia maisha yao jambo ambalo litasababisha kupatikana kwa kizazi kizuri hapo baadaye.
Kamati hiyo imekutana kwa mara ya pili
kwa ajili ya kupitia rasimu ya maazimio ya kuhakikisha kuwa vijana wote katika
nchi zilizopo ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kusini wanapata elimu kuhusiana
na afya ya uzazi na ujinsia jambo ambalo litawasaidia kufahamu zaidi ugonjwa Ukimwi kwamara ya kwanza ilikutana mwezi
wa nane nchini Botswana.
Makubaliano hayo
yanatarajiwa kusainiwa na mawaziri wa Afya na Elimu kutoka nchi 21 za
Afrika Mashariki na Kusini ambayo inatakuwa ni sehemu ya utekelezaji kwa nchi kabla
ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na magonjwa
ya zinaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni mjini humo.
No comments:
Post a Comment