Tanzanite
imesema iko vizuri kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kwa
wasichana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Afrika Kusini
(Basetsana) inayochezwa kesho Jumamosi (Desemba 7 mwaka huu) Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Kocha
Mkuu wa Tanzanite, Rogasian Kaijage amesema wamejiandaa vizuri kwa
mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa kuanzia saa 10
kamili jioni.
“Tumejiandaa,
vijana wako vizuri wanasubiri saa ya mechi tu. Licha ya kwamba Afrika
Kusini wako mbele kwenye mpira wa miguu wa wanawake si sababu ya
matokeo,” amesema Kaijage.
Amesema
anaamini vijana wake watafanya vizuri, na kuwataka Watanzania
wajitokeze kwa wingi kuwashangilia ili waweze kupata matokeo mazuri
kwenye mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na msisimko mkubwa.
Naye
nahodha wa Tanzanite, Fatuma Issa amewataka Watanzania kuwaamini kwani
wamejipanga kwa ajili ya pambano hilo, hivyo wawe nyuma yao katika
kuwaongezea ari ili waweze kufanya vizuri.
Viingilio
katika mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na
orange, sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A watalipa
sh. 10,000. Tiketi zitauzwa uwanjani katika magari maalumu.
Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
RAMBIRAMBI MSIBA WA NELSON MANDELA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Rais
wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela kilichotokea jana (Desemba 5
mwaka huu) nchini humo.
Msiba
huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwa Afrika Kusini,
Afrika na Dunia kwa ujumla kutokana na mchango mkubwa wa Mzee Mandela
katika mchezo huo.
Mzee
Mandela anakumbukwa kwa mchango wake katika Fainali za Afrika (AFCON)
zilizofanyika mwaka 1996 nchini Afrika Kusini na hata zile za Kombe la
Dunia zilizofanyika nchini humo mwaka 2010.
TFF
tunatoa pole kwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA),
Danny Jordan, na wananchi wa Afrika Kusini na kuwataka kuwa na subira
na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Mandela mahali pema peponi. Amina.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment