Na Anna Nkinda –
Maelezo, Lindi
Wakazi wa mkoa
wa Lindi wametakiwa kutodanganyika na kundi la watu wachache wanaotaka kuvuruga
amani iliyopo bali waitunze na kuhakikisha kuwa haipotei kwani amani ikitoweka
hao wanaowadanyanga watakimbia na kuwaacha wakiteseka .
Wito huo umetolewa leo
na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa
wakati wa uzinduzi wa sherehe za kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinnduzi (CCM) mkoani
Lindi zilizofanyika katika kata ya Kiwalala wilaya ya Lindi vijijini ambapo
chama hicho kinatimiza miaka 37.
Mama Kikwete alisema
CCM imefanya mambo mengi katika harakati za ukombozi Barani Afrika kwani
Tanzania ilikuwa kimbilio la wanyonge kwa kuwa wapigania uhuru wengi kutoka
nchi za Kusini mwa Afrika ambazo hazikuwa zimepata uhuru walipokelewa , walihifadhiwa
, walisaidiwa na kuwakarimu kwa dhati jambo ambalo si dogo na hii yote
ilitokana na amani iliyopo.
“Chama chetu
kimefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na
kuleta Demokrasia ya vyama vingi toka mwaka 1992 na leo hii tunatimiza miaka 22
ndani ya mfumo wa vyama vingi huku tukiwa na amani, umoja na ushikamano
miongoni mwa watanzania, tumeleta usawa kwa wananchi wote bila kujali jinsia,
rangi kabila wala dini.
Chama cha Mapinduzi
kupitia Serikali zake zinawajali wananchi kwa kuwasogezea huduma mbalimbali za
kijamii hadi vijijini na kupanua fursa
za kiuchumi na kimaendeleo kwa wananchi”, alisema Mke wa Rais.
Aidha Mjumbe huyo wa
NEC pia aliwataka wananchi hao kujishughulisha
na kazi mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kulima japo mazao ya chakula kama muhogo kwani
Serikali tayari imeshafanyia mambo mengi ya maana ambayo yanawasaidia katika shughuli zao za maendeleo.
Mama Kikwete alisema, “Serikali
imejenga Shule, Hospitali, barabara na kuimarisha miundombinu ya barabara na leo hii kama mtalima kwa bidii mtaweza
kusafirisha na kuuza mazao yenu mbali na
hapa kwakuwa barabara ni nzuri na usafiri ni wa uhakika”.
Kwa upande wake Mlezi
wa Chama hicho katika mkoa wa Lindi Dk. Maua Daftari aliwataka wanachama wa
chama hicho kuwa na umoja na mshikamano kwa kufanya hivyo wataweza kushinda na kutekeleza
ilani ya chama chao.
Katika uzinduzi wa
sherehe hizo ambazo kilele chake
kitafanyika kesho katika wilaya ya
Ruangwa jumla ya wanachama 17 walijiunga na chama hicho ambapo wanachama wapya
ni 12, kutoka chama cha upinzani cha Civic United Front (CUF)
wanne na Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) mmoja.
No comments:
Post a Comment