Na Beatrice Lyimo-
MAELEZO.
Dar es
salaam.
Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inatarajia kufanya kampeni
shirikishi ya ugonjwa wa Surua na Rubella kuanzia tarehe 18 hadi 24 oktoba,
2014.
Akizungumzia kampeni
hiyo itakayofanyika nchini nzima leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa
wizara hiyo Dkt. Donan Mmbando amesema kuwa itawahusisha watoto wenye umri wa
kuanzia miezi 9 hadi miaka 15.
Amesema kampeni hiyo
itaambatana na utoaji wa matone ya Vitamini A, dawa za kutibu na kukinga
magonjwa ya Minyoo, Usubi,Matende na Mabusha.
Dkt. Mmbando amesema
kuwa lengo na madhumuni ya kampeni hiyo ni kudhibiti milipuko ya magonjwa ya
Surua na Rubella ili kupunguza vifo na madhara yanayosababishwa na magonjwa
hayo.
“Katika kampeni hii
tutatoa dawa za kutibu na kukinga magonjwa ya Minyoo, Usubi, Matende na Mabusha
katika mikoa 16 yenye maambukizi makubwa ya magonjwa haya”, Amesisitiza Dkt. Mmbando.
Amefafanua kuwa chanjo ya
Surua na Rubella itatoa fursa ya kutoa kinga kwa watoto wengi zaidi ambao
hawakupata chanjo hiyo utotoni katika mikoa yenye maambukizi makubwa ya
magonjwa hayo ambayo ni Mtwara, Lindi, Tanga , Dar es salaam,Morogoro, Pwani, Tabora, Manyara,
Iringa, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Singida, Dodoma na Njombe.
Akitoa ufafanuzi kuhusu
chanjo hizo amesema kuwa chanjo ya Surua na Rubella itatolewa kwa watoto wenye
umri wa miezi 9 hadi chini ya miaka 15, matone ya vitamin A kwa watoto wenye
umri wa miezi 6 hadi chini ya miaka 5.
Nyingine ni dawa za
minyoo (Mebendazole) zitakazotolewa kwa watoto wenye umri wa miezi 12 hadi
chini ya miaka 5 nchi nzima na dawa za kutibu na kukinga minyoo (Albendazole)
Usubi, Matende na mabusha au Ngirimaji kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 5
na kuendelea katika mikoa 16 iliyobainishwa.
Kwa upande wake Meneja
Mpango wa Taifa wa Chanjo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Dafrosa Lyimo ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha
kuwa wanawapeleka watoto wao katika vituo vya afya ili waweze kupata chanjo hiyo.
Pia ametoa wito kwa
mama wajawazito kuhakikisha kuwa wanapata chanjo ya Surua-Rubella ili kuwakinga
watoto wao dhidi ya matatizo ya Moyo, mimba kuharibika, kujifungua kabla ya
wakati na mtindio wa ubongo yanayotokana na ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment