Na
Veronica Kazimoto
Morogoro
Wito umetolewa kwa
Maafisa wa Ngazi za Juu wa Jeshi la Magereza kutoka vitengo mbalimbali vya
Makao Makuu ya Jeshi hilo kuwahimiza maofisa waliopo chini yao kutumia takwimu
mbalimbali zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ili zisaidie katika
kuandaa mipango na kutoa maamuzi mbalimbali ya kazi zinazofanywa na jeshi hilo.
Wito huo umetolewa leo
na Meneja Tawala wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Gabriel Madembwe wakati
akifungua Mafunzo ya Takwimu Rasmi kwa Maafisa wa Ngazi za Juu wa Jeshi hilo yaliyofanyika
katika ukumbi wa Amabilisi uliopo mkoani Morogoro.
Madembwe amesema kuwa maafisa
wengi katika Jeshi la Magereza wakijua umuhimu wa matumizi ya takwimu itasaidia
kuleta mabadiliko hasa katika kupanga mipango yao kwenye maeneo yao ya kazi.
"Napenda
kusisitiza kuwa ili mabadiliko yatokee sehemu yoyote ile; iwe nyumbani, kazini au katika jamii, ni lazima kuwepo na
kichocheo cha mabadiliko hayo, hivyo ninyi mtakuwa kiungo muhimu katika kuleta
mabadiliko yenye kutoa maamuzi kwa kuzingatia matumizi ya takwimu rasmi",
amesema Madembwe.
Nae Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka Makao Makuu Dar es Salaam Bw. Edward
Kaluvya amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo kwa sasa wamekuwa
wakitumia sana takwimu katika maeneo mengi ya kazi zao.
"Mafunzo haya
yatatusaidia kujenga uelewa wa pamoja na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali
yanayohusiana na uzalishaji, uhifadhi na utumiaji wa takwimu kwa usahihi katika
kutoa maamuzi na kupanga mipango endelevu katika Jeshi letu la Magereza'',
amefafanua Kaluvya.
Mafunzo haya ya siku
tatu yanatolewa na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika kilichopo jijini Dar
es Salaam na yamefadhiliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupia Mpango Kabambe wa
Kitaifa wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu Tanzania (TSMP).
Lengo kuu la Mpango huu
ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo imara wa kitaifa wa kuratibu,
kukusanya, kuhifadhi na kusambaza takwimu nchini.
Meneja Tawala wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu,Gabriel Madembwe (katikati) akiwahutubia Maafisa wa Ngazi za Juu wa Jeshi la
Magereza kutoka vitengo mbalimbali vya Makao Makuu ya Jeshi hilo wakati wa
ufunguzi wa Mafunzo ya Takwimu Rasmi yaliyofanyika mkoani Morogoro. Kushoto
ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Dk, Frank Mkumbo na kulia ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Jeshi la Magereza Makao Makuu Edward Kaluvya.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakichukua habari
wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Takwimu Rasmi kwa Maafisa wa Ngazi za Juu wa
Jeshi la Magereza kutoka vitengo mbalimbali vya Makao Makuu ya Jeshi hilo
yaliyofanyika katika ukumbi wa Amabilisi uliopo mkoani Morogoro.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika
Dk, Frank Mkumbo akiwa katika mahojiano
na Waandishi wa Habari mara baada ya ufunguzi wa Mafunzo ya Takwimu Rasmi kwa
Maafisa wa Ngazi za Juu wa Jeshi la Magereza kutoka vitengo mbalimbali vya Makao
Makuu ya Jeshi hilo yaliyofanyika katika ukumbi wa Amabilisi uliopo mkoani
Morogoro.
No comments:
Post a Comment