Timu ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa
ufukweni (beach soccer) imepangiwa kucheza na Kenya katika raundi ya kwanza ya
michuano ya Afrika kwa ajili ya fainali za Afrika za michuano hiyo zitakazofanyika
Aprili mwaka huu nchini Shelisheli.
Mwenyekiti wa Kamati ya Beach Soccer,
Ahmed Idd Mgoyi amesema jijini Dar es Salaam, leo kuwa Tanzania itaanzia
ugenini ambapo mechi ya kwanza itachezwa kati ya Februari 13 na 15 mwaka huu
nchini Kenya.
Mechi ya marudiano itafanyikaa nchini
kati ya Februari 20 na 22 mwaka huu. Iwapo timu ya Tanzania itasonga mbele,
katika raundi ya pili itacheza na Misri ikianzia nyumbani kati ya Machi 13 na
15 mwaka huu.
Mgoyi alisema maandalizi ya Tanzania
kushiriki kwenye mashindano hayo yameanza ambapo timu ya Tanzania Bara itacheza
na Zanzibar ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kupata kikosi kimoja kitakachoingia
kwenye michuano hiyo ya Afrika.
Alisema benchi za ufundi la timu ya
Tanzania litaongozwa na John Mwansasu wakati Msaidizi wake ni Ali Shariff
'Adolf' kutoka Zanzibar, na Meneja wa timu hiyo ni George Lucas. Wote hao
walishiriki kwenye kozi ya ukocha wa beach soccer iliyoendeshwa mwaka jana
nchini na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kocha Mwansasu atatangaza timu ya
Tanzania Bara, Januari 19 mwaka huu, na mazoezi ya pamoja na timu ya Zanzibar yatafanyika
Januari 24 na 25 mwaka huu.
Wachezaji wa timu ya Tanzania Bara
watatokana na michuano ya beach soccer iliyofanyika mwaka jana ikishirikisha
timu za vyuo vya elimu ya juu vya Mkoa wa Dar es Salaam.
POLISI MARA YAZUIWA KUCHEZA UWANJA WA KARUME MUSOMA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeizuia timu ya
Polisi Mara kutumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma kwa mechi zake
za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuanzia leo mpaka hapo itakapotangazwa
vinginevyo.
Uamuzi huo umechukuliwa kutokana na matukio ya vurugu na uvunjifu
wa amani ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mechi za FDL zinazochezwa kwenye
uwanja huo, ikiwemo ile ya Jumamosi iliyopita dhidi ya Mwadui ya Shinyanga
ambapo waamuzi walipigwa.
Kamati zinazohusika zitakutakana hivi karibuni kupitia matukio
yote ya utovu wa nidhamu kwenye FDL, na hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika
ikiwemo na viwanja ambavyo vimekuwa na sifa ya vurugu.
Vyama vya mpira wa miguu vya mikoa vina wajibu wa kutoa ulinzi wa
kutosha viwanjani wakati wa mechi.
RAUNDI YA PILI TAIFA CUP WANAWAKE JUMAMOSI
Mechi za kwanza za raundi ya pili ya mashindano ya Taifa ya mpira
wa miguu kwa wanawake (Taifa Cup Wanawake) zinachezwa wikiendi hii (Januari 17
mwaka huu) kwenye miji minane tofauti nchini.
Timu tisa zilizofuzu kutoka raundi ya kwanza baada ya mechi za
nyumbani na ugenini akiwemo mshindwa bora (best loser) zitaungana na Ilala, Kinondoni
na Temeke kucheza raundi ya pili. Mechi za marudiano za raundi hiyo zitachezwa
Januari 21 mwaka huu.
Hatua ya robo fainali itakayochezwa Januari 26 na 27 mwaka huu
pamoja na nusu fainali na fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Proin
Promotions itafanyikia jijini Dar es Salaam.
KOCHA
NOOIJ KUTAJA STARS MABORESHO
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij anatarajia kutaja kikosi cha
Maboresho kitakachoingia kambini Januari 18 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya
kirafiki dhidi ya Rwanda itakayofanyika Januari 22 mwaka huu jijini Mwanza.
Nooij atataja kikosi hicho kwenye mkutano na waandishi wa habari
utakaofanyika kesho (Januari 15 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Uwanja wa Karume.
RAMBIRAMBI MSIBA WA STEPHEN NSOLO
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa Katibu Mkuu wa zamani wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) uliotokea jana (Januari 13
mwaka huu) jijini Mwanza.
Msiba huo ni pigo kwa wadau wa mpira wa
mpira wa miguu kwani wakati wa uhai wake, Nsolo alitoa mchango mkubwa akiwa
kiongozi. Aliongoza SHIREFA akiwa Katibu kuanzia mwaka 1975 hadi 1994.
Kabla ya hapo alikuwa Katibu wa Chama
cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Shinyanga kwa kipindi cha miaka kumi. Pia aliwahi
kuwa mwamuzi wa daraja la kwanza na kamishna wa mpira wa miguu kwa muda mrefu.
TFF inatoa salamu za rambirambi kwa
familia ya marehemu, SHIREFA na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania
(FRAT) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa
msiba huo.
Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo
(Januari 14 mwaka huu) katika makaburi ya Shinyanga Mjini. Bwana alitoa, Bwana
ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment