Na
Mwandishi Wetu.
Dar
es Salaam.
WADAU wa tasnia ya
habari nchini wametakiwa kujiepusha na itikadi
za kisiasa kwa kisingizio cha ufinyu wa
muda katika kujadili muswada wa sheria ya huduma za habari kwa kuwa
sheria si kitabu takatifu kisichoweza kufanyiwa marekebisho.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka wakati wa
mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi.
Mtaka alisema Muswada
wa Sheria ya Huduma za Habari ni mjadala wa miaka mingi ambao kwa kipindi
kirefu wadau wa habari wakiwemo Wamiliki, Wahariri, vyama vya taaluma na
waandishi wa habari wamekuwa wakilumbana
na Serikali pasipo kupatikana kwa suluhu
ya kudumu.
Kwa mujibu wa Mtaka
alisema Tanzania haitokuwa Nchi ya kwanza duniani kutunga sheria na kuibadilisha, hivyo
aliwataka wadau wa habari kutambua kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya
kusaidia tasnia hiyo tofauti na tafsiri mbalimbali zinatolewa na wadau hao
kuhusu muswada huo.
“Wanahabari
wanapoujadili muswada huu, wanapaswa kuangalia leo na kesho kwani Serikali
ilitoa kipindi kirefu cha kujadili na wadau waliwasilisha maoni yao, wasiwasi
unatoka wapi kuhusu muswada huu” alisema Mtaka.
Aliongeza kuwa kabla
ya muswada huo kuwasilishwa kwa mara ya kwanza Bungeni, baadhi ya wamiliki na
wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari walikuwa mafundi wa kuandika makala na
tahariri zilizoishutumu Serikali kuwa inachelewesha muswada huo bila sababu za
msingi.
Aidha ,Mtaka
aliongeza kuwa kupatikana kwa sheria mpya itayotokana na muswada itasaidia
kufutwa kwa sheria mbalimbali zinazoongoza tasnia hiyo ikiwemo sheria ya
magazeti ya mwaka 1976 ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa ikilalamikiwa na wadau
wa habari kuwa ni sheria kandamizi kwa ustawi wa vyombo vya habari nchini.
Akizungumzia kuhusu
Ibara ya 7 ya muswada huo inayozungumzia kuhusu Wajibu wa vyombo vya habari
kutangaza na kuandika habari zinazohusu maslahi ya taifa, Mtaka alisema
kipengele hicho hakikusudii kuminya uhuru wa vyombo binafsi vya habari.
Alisema kwa
kuzingatia kuwa vyombo vya habari ni mhimili wa nne wa dola, ni wajibu wa
taasisi za habari kutangaza na kuandika habari zinazozingatia maslahi ya nchi
na wananchi kwa ujumla wake.
Kuhusu uhuru wa
habari kutambuliwa katika Katiba ya nchi, Mtaka alisema wahariri na waandishi
wa habari wamekuwa wakiitafsiri vibaya ibara ya 18 ya Katiba na kusahau Ibara
ya 31 inayoeleza mipaka inayopaswa kuzingatiwa katika kutafuta, kupokea na
kusambaza taarifa.
Kuhusu kipengele cha
leseni kwa waandishi wa habari, Mtaka alisema wakati umefika kwa tasnia ya
habari kuwa na heshima kama zilivyo taaluma nyingine ambazo wadau wake
hupewa leseni inayowawezesha kutambulika
na Bodi za kitaaluma.
Mtaka alisema
utaratibu huo ni vyema ukaanzia ndani ya vyombo vya habari vyenyewe ikiwemo
nafasi ya Mhariri wa gazeti/televisheni au redio ni vyema awe na leseni ya
kazi, hatua itayosaidia kuongezea hadhi na sifa ya tansia hiyo.
“Ukianzisha utaratibu
kama huu, utasaidia kuongeza morali ya wanahabari sasa kwenda kusoma na hiyo
itasaidia kuwaongezea weledi katika taaluma” alisema Mtaka.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara, Hamis
Dambaya aliwataka wadau wa habari kufanya maridhiano ya pamoja na Serikali badala ya kupinga muswada huo.
Alisema kwa muda
mrefu muswada huo ulikuwa mikononi mwa wadau wa habari, ambao kwa kipindi
kirefu wamekuwa wakilalamikia kukosekana chombo cha kusimamia taaluma hiyo,
ambapo muswada umependekeza kuanzishwa
Baraza huru la Habari ambalo litasimamia haki, wajibu na miiko ya tasnia hiyo.
“Wadau hawatakiwi
kuweka mikwamo pasipo na kufahamu mbele kuna nini, ni vyema sasa suala hili
likafikia mwisho ili sheria iweze kutungwa na hatimaye tasnia ya habari ikapata
hadhi na heshima kama zilivyo taaluma nyinge” alisema Dambaya.
No comments:
Post a Comment