Na Anna Nkinda – Maelezo Dar
es Salaam
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amepongezwa kwa
jitihada zake za kuinua sekta ya michezo nchini jambo ambalo
limewafanya vijana wengi kujipata ajira katika fani hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Lindi (LIREFA)
Francis Ndulane wakati wachezaji wa timu ya Kariakoo ya mkoa huo
walipozitembelea ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizopo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Ndulane alisema kuwa mchango unaotolewa na Mama Kikwete umewapa hari na kuwatia moyo vijana wengi na hivyo kuweza kuendeleza sekta ya michezo mkoani humo.
Alisema
kuwa hapa nchini vijana wengi wana vipaji mbalimbali, lakini hawana
watu wa kuwaendeleza, hivyo alimshukuru kwa jitihada zake za
kuwaendeleza katika sekta hiyo na hivi sasa wanaamini kuwa wataweza kujiajiri na kuweza kuzisaidia familia zao.
Kwa
upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA
aliwapongeza wachezaji hao kwa juhudi kubwa wanayoifanya katika soka
hadi kufikia hatua ya kushiriki ligi ya taifa ya mabingwa wa mkoa ngazi
ya taifa na kufikia hatua ya nane bora.
Naye
Mwenyekiti wa timu hiyo Abdalah Livemba aliwashukuru Mama Kikwete na
Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe kwa moyo walionao wa kuisaidia timu
hiyo hadi kufikia hapo ilipo.
Alimuomba kuwatafutia mdhamini ili awezkuwasaidia kubeba mzigo mkubwa wa kuitunza timu hiyo ambao unaelekea kuwalemea.
Mama Kikwete aliikabidhi timu hiyo zawadi za viatu pea 29, jezi seti mbili ambazo ni 32, mipira mitatu, pampu moja na soksi pea 16.
Timu
ya Kariakoo inashiriki mashindano ya ligi ya mabingwa mkoa ngazi ya
Taifa ambayo yalianza tarehe 12/6/2013 kwa kuzishirikisha timu
28 kutoka nchi nzima wao wamebaki kati ya timu nane na leo wanapambana
na Friends Rangers ya mkoa wa Dar es Salaam mchezo utakaofanyika katika
uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment